1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

China yaishutumu Marekani kwa kuipaka tope

27 Mei 2022

Wizara ya mambo ya nje ya China siku ya Ijumaa imemshutumu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken", baada ya kutoa hotuba inayotaka kuchukuliwa hatua kukabiliana na ushawishi wa Beijing.

https://p.dw.com/p/4Bxok
Außenminister Antony Blinken spricht im Jack Morton Auditorium der George Washington University über China
Picha: Alex Wong/AFP

Katika hotuba hiyo iliyosubiriwa kwa muda mrefu, Blinken alisema China imeleta "changamoto ya muda mrefu kwa utaratibu unaokubalika kimataifa". China imepewa tahadhari hivi karibuni kutoka kwa Marekani na washirika wa Magharibi kuhusu ushawishi wake unaoongezeka na mahitaji ya ulimwengu.

Katika hotuba yake siku ya Alhamisi, Blinken alitahadharisha kuhusu  "nia ya China ya kuunda upya utaratibu wa kimataifa" na kuzitaka nchi kulinda mambo yake ya ndani. Pia aliishutumu China kwa kuibua mvutano juu ya Taiwan, kisiwa kinachojitawala ambacho China inadai kuwa eneo lake  na kusema kuwa China "imekata uhusiano wa Taiwan na nchi nyingine duniani kote na inaizuia kushiriki katika mashirika ya kimataifa".

China imeikashifu hotuba hiyo, ikisema "inaeneza habari za uongo kuhusu  China, inaingilia mambo ya ndani ya China, na inachafua sera za ndani na nje za China". Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Wang Wenbin aliwaambia waandishi wa habari kwamba China "inapinga vikali" hotuba hiyo na imeonyesha kuwa Marekani inataka "kurudisha nyuma maendeleo ya China na kudumisha utawala wa  Marekani".

Hivi karibuni Marekani imezindua mfumo mpya wa kibiashara na mataifa ya barani Asia na kuanzisha jukwaa la pamoja na Umoja wa Ulaya litakaloweka viwango vinavyokubalika katika sekta ya teknolojia. Juhudi hizo zinalenga kuunganisha mataifa yenye nia moja na kuipiku China ambaye imekuwa ikitawala kwenye sekta ya teknolojia mpya kama vile teknolojia ya Akili Bandia.

Hotuba yatofautiana na enzi ya Trump

Hotuba ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani imetofautiana na mbinu iliyotumika na utawala uliopita wa Marekani wa rais wa zamani Donald Trump, ambapo ulizungumza kwa uthabiti kuhusu mzozo wa pande zote za dunia na China.

Katika ziara yake  Afrika na Amerika ya Kusini, ambako China imewekeza mabilioni ya dola katika miundombinu, Blinken amepuuza ushindani wa Marekani na China na hajaomba mataifa kuchukua upande."Hatutarajii mzozo au vita baridi vipya. Kinyume chake, tumedhamiria kuepukana na yote mawili," alisema katika hotuba yake.

"Hatudhamirii kuizuia China kwenye jukumu lake kama taifa lenye nguvu,au kuizuia nchi nyingine kwa jambo hilo kukuza uchumi wao au kuendeleza maslahi ya watu wao."

Lakini alisema kwamba kutetea utaratibu wa sasa wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na sheria na makubaliano ya kimataifa, "kutapelekea uwezekano kwa nchi zote ikiwa ni pamoja na Marekani na China kuishi pamoja na kushirikiana".

Siku ya Jumatatu, Biden alitoa ahadi ya wazi kwamba katika miongo kadhaa Marekani itailinda Taiwan kutokana na uvamizi wowote wa  China. Ahadi hiyo imepelekea China, kuitahadharisha Marekani  "kutodharau" uwezo wa China.

Siku ya Alhamisi Biden alisisitiza kuwa Marekani haibadilishi  msimamo wake wa muda mrefu kuhusu Taiwan na kusema kuwa China ndiyo imeibua mvutano, ikiwa ni pamoja na safari za  kila siku za kijeshi karibu na kisiwa hicho.

(afp)