China, Pakistan, Afghanistan | Magazetini | DW | 05.09.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

China, Pakistan, Afghanistan

Kwa mara nyingine tena zipo mada mbalimbali katika udondozi wa magazeti hii leo. Suala la kwanza ni juu ya upelelezi wa Wachina kwenye kompyuta za serikali ya Marekani ambao umegunduliwa hivi karibuni.

Mhariri wa “Obermain-Tagblatt” anakumbusha juu ya maneno ya mzee wa kichina aliyekuwa na busara Konfuzius na ameandika:

“Wachina wanaamini mno katika matamshi ya Konfuzius yanayosema: bila ya kwenda njia ambayo wengine wameichukua hutafikia lengo. Wakitumia njia ya mtandao wa komyputa, Wachina sasa wamefika hadi ndani ya wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon kwa azma ya kupepeleza wizara hiyo. Kwa hiyo, vita vya kikompyuta vimeanza. Kwa kweli, biashara ya kimataifa iko hatarini iwapo kachero wa kompyuta wakiagizwa na serikali fulani watapeleleza siri za kijeshi na kiuchumi za nchi nyingine.”

Zaidi juu ya shambulio hili dhidi ya kompyuta za wizara ya ulinzi ya Marekani tunasoma katika gazeti la kichumi la “Handelsblatt”:

“Bila shaka, Marekani haitasema wazi kwa kiwango gani Wachina waliweza kupeleleza katika kompyuta zake. Kwani inaonyesha kwamba wizara haikujikinga vizuri. Juu ya hayo, uhusiano kati ya Marekani na China tayari si mzuri sana na unaweza kuathirika zaidi ikiwa data zinapelelezwa na kuibwa.”

Tugeukie katika la pili ambalo linazingatiwa katika gazeti la “Frankfurter Rundschau”. Mhariri huyu anaeleza wasiwasi wake juu ya hali nchini Pakistan na anatoa mwito kwa nchi za Ulaya na Marekani wasiyaweke kando matukio huko Pakistan, kwani:

“Nchi hii ambayo ni mshirika wa karibu katika vita dhidi ya ugaidi inaweza kuingia katika hali ya machafuko, si tu kutokana na mashambulio ya kigaidi, bali pia kwa sababu hali ya kisiasi si wazi. Rais Musharraf, badala ya kuwa mwindaji, sasa yeye mwenyewe anawindwa na wengine. Na vilevile kurudi kwa wanasiasa maarufu wa upinzani Benazir Bhutto na Nawaz Sharif hakutatuliza hali. Hawa wawili, sasa, wanajifanyia kuwa ni waokozi wa demokrasia, hata hivyo wakati katika miaka yao walipokuwa madarakani wao wenyewe hawakuifuata demokrasia halisi.”

Na hatimaye ni juu ya nchi nyingine ambapo vita vinaendelea, yaani Afghanistan. Leo hii, kama tulivyosikia awali katika ripoti baraza la mawaziri la Ujerumani linatarajiwa kuamua juu ya mbinu mpya ya serikali ya nchi hiyo wa kuelekea Afghanistan, kabla ya bunge baadaye mwezi huu litakapoamua juu ya kurefusha muda wa jeshi la Ujerumani kubaki huko Afghanistan. Ufuatao ni uchambuzi wa mhariri wa “Süddeutsche Zeitung” kuhusu mbinu mpya ya serikali:

“Katika mswada juu ya sera za kuelekea Afghanistan, serikali inaweka picha halisi ya hali ilivyo. Bila ya kutumia lugha ya kidiplomasia inaelezea msingi wa kutokuwa na mafanikio, yaani rushwa na biashara ya madawa ya kulevya nchini Afghanistan. Bila ya kuficha chochote inakiri wapi imeshindwa katika kujenga upya usimamizi na polisi. Kwa kuzungumzia wazi makosa yaliyofanywa, serikali hiyo pia imeweza kuonyesha kwamba matokeo yatakuwa mabaya zaidi ikiwa nchi za Magharibi zitaondoa haraka msaada wake. Katika sera zake, serikali ya Ujerumani inahitaji kuungwa mkono na wananchi. Mswada huu ambao unasema ukweli ni hatua ya kwanza kuupata ungwaji mkono huu.”

 • Tarehe 05.09.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHRv
 • Tarehe 05.09.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHRv
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com