1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto ya mitaala katika vyuo vya biashara Afrika

Anuary Mkama22 Mei 2018

Shirikisho la vyuo vya biashara barani Afrika limetaka mitaala kufanyiwa mabadiliko ili iendane na mahitaji yaliyopo katika jamii

https://p.dw.com/p/2y7kb
Tansania dLab
Picha: DW/V. Natalis

Shirikisho la vyuo vya biashara barani Afrika limekiri kuwa kuna changamoto ya mitaala ya kufundishia hivyo limezitaka baadhi ya nchi wanachama wa shirikisho hilo kufanya mabadiliko ili mitaala hiyo iende sambamba na mahitaji yaliyopo katika jamii.

Hayo yameelezwa katika ufungaji wa kongamano la shirikisho hilo lia jijini Dar es Salaam, Tanzania na kushirikisha vyuo 25 kutoka mataifa mbalimbali Afrika.

Kumekuwepo na mijadala kuhusiana na kupitiwa kwa mitaala ya masomo mbalimbali hususan katika elimu ya juu ili mitaala hiyo iende sambamba na kile ambacho kipo katika jamii lakini pia kutoa fursa kwa wahitimu kujiajiri.

Mitaala haiendi sambamba na sera ya mipango ya uchumi?

Katika kongamano linalofanyika kila mwaka la shirikisho la vyuo vya biashara Afrika ambalo limemalizika Jumanne mjini  Dar es Salaam, wanachama wa shirikisho hilo wamekiri kuwa kuna kila haja ya kufanya mabadiliko ya mitaala yao wanayotumia kufundishia kwani haiendani na sera ya mipango ya kiuchumi ya mataifa yao lakini pia mahitaji ya jamii kwa ujumla.

Wito umetolewa wa kuwa na muunganiko baina ya vyuo vya biashara na serikiali
Wito umetolewa wa kuwa na muunganiko baina ya vyuo vya biashara na serikialiPicha: DW/K. Makoye

Maazimio yaliofikiwa  ni kuhakikisha tafiti ambazo zimekuwa zikifanywa katika vyuo hivyo na wanataaluma ziwe zina mchango wa moja kwa moja katika maendeleo ya nchi hususan katika sekta ya biashara na uchumi na kuachana na tafiti ambazo zimekuwa zikiwavusha kitaaluma wale wanaozifanya lakini pia vyuo hivyo vya biashara vimekubaliana kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili kwa pamoja ikiwemo uhaba wa rasilimali watu ambao umeleezwa kuwa ni changamoto kubwa kwa vyuo mbalimbali hususan vile ambavyo ni vya umma.

Wahitimu kutoka Afrika wana viwango sawa vya ubora?

Kwa upande wake Profesa Justice Bawole wa Chuo Kikuu cha Ghana amesema wakati umefika wa wahitimu wa masomo ya biashara wa mataifa ya Afrika wawe na kiwango sawa cha ubora ili kuwapa fursa ya kupambana katika soko la ajira la Afrika na Dunia nzima kwa ujumla.

Maazimio mengine yaliyofikiwa katika kongamano hilo ni kuhakikisha kuna kuwa na muunganiko baina ya vyuo vya biashara na serikiali hususani katika mipango yake ya kiuchumi ili kuwapata wahitimu ambao wataenda moja kwa moja katika shughuli ambazo serikali imezipanga katika mipango yake kama ilivyo kwa uchumi wa viwanda nchini Tanzania

Miongoni mwa mataifa yalihudhuria kongamano hili ni Afrika Kusini, Morocco, Senegal, Kenya, Ghana na mengineyo wanachama wa shirikisho hilo ambalo mkutano wake ujao unatarajiwa kufanyika nchini Afrika Kusini mwakani.

Mwandishi: Anuary Mkama

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman