Chama cha Labour Uingereza chaandikisha matokeo mabaya
9 Mei 2026
Matokeo ya mwisho yaliowasilishwa leo Jumamosi, yameonyesha kuwa chama cha Labour kimepoteza viti 1,000 vya udiwani kote Uingereza na kuondolewa mamlakani huko Wales baada ya kuongoza kwa miaka 27.
Chama kinachopinga uhamiaji cha Reform UK kimeshinda karibu viti 1,300 kote nchini Uingereza, huku kikishika nafasi ya pili huko Wales na kupata mafanikio makubwa nchini Scotland.
Matokeo hayo yanaonekana na wengi kama kura ya maoni isiyo rasmi dhidi ya Starmer, ambaye umaarufu wake umeshuka tangu alipochukuwa uongozi wa chama hicho cha Labour takriban miaka miwili iliyopita.
Hata hivyo hii leo, Starmer amesisitiza kuwa hataondoka na kuitumbukiza nchi hiyo katika mparaganyiko, na kusema kwamba matokeo hayo hayajaleta changamoto ya moja kwa moja kwa uongozi wake.