Berlin na Hamburg kuwania tikiti ya kuandaa Olimpiki | Michezo | DW | 28.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Berlin na Hamburg kuwania tikiti ya kuandaa Olimpiki

Miji miwili mikubwa ya Ujerumani Berlin na Hamburg mwezi ujao itawasilisha maombi yao ya kutaka kuwa wenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya mwaka wa 2024. Jee, itakuwa Berlin au Hamburg itakayopewa kibali?

Shirikisho la Michezo ya Olimpiki la Ujerumani pia litaamua kama litatangaza ombi la kuandaa michezo hiyo katika mwaka wa 2018 au la.

Miji yote miwili itazindua mawazo yao na kujibu maswali kutoka kwa Shirikisho la Michezo ya Olimpiki la Ujerumani –DOSB mnamo Septemba mosi, kabla ya uamuzi wa mwisho kuchukuliwa Desemba 6.

Meya wa Berlin Klaus Wowereit, amesema ana matumaini kuwa watayajibu maswali hayo vyema. Baada ya miji hiyo kuwasilisha mipango yao ya kuandaa michezo hiyo, kutakuwa na kura kutoka kwa raia wote wa miji hiyo.

Berlin iliandaa kwa mara ya mwisho michezo ya Olimpiki mnamo mwaka wa 1936 wakati wa kipindi cha utawala wa Nazi. Awamu ya kutuma maombi rasmi kwa ajili ya kuandaa michezo ya Olimpiki ya 2024 inaanza mwaka ujao huku umauzi ukifanyika mwaka wa 2017.

Hakuna miji mingine iliyotangaza nia ya kutaka kuandaa mashindano hayo kufikia sasa lakini kuna uwezekano kuwa miji ya Marekani ya Los Angeles na Boston, pamoja na Paris na Istanbul inaweza kuwasilisha maombi yao. Michezo ijayo ya Olimpiki itaandaliwa katika mji wa Rio de Janeiro nchini Brazil mwaka wa 2016 na Tokyo, Japan mwka wa 2020.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Grace Patricia Kabogo