Barack Obama ziarani Israel | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Barack Obama ziarani Israel

Mgombea kiti cha urais kutoka chama cha demokrate nchini Marekani Barack Obama sasa yupo nchini Israel kwa mazungumzo na viongozi wa Israel na Palestina.

default

Seneta Barack Obama

Mara tu baada ya kuwasili mjini Tel Aviv nchini Israel akitokea Jordan, Barack Obama alisema kitu muhimu kwake ni kuthibitisha uungwaji wake mkono kwa Israel na sio tu kwa kuendeleza uhusiano maalum na tena wa kihistoria kati ya Marekani na Israel bali pia kuuimarisha. Barack Obama amewasili nchini Israel masaa machache baada ya mpalestina moja kuwajeruhi watu 16 mjini Jerusalem kwa kutumia tingatinga alilokuwa akiliendesha kabla ya kuuliwa na polisi wa usalama. Barack Obama amelaani kitendo hicho kwa kusema: ´´Ninalaani vikali shambulio hilo na nitaiunga mkono Israel katika kupambana na ugaidi na kuendeleza juhudi za amani na usalama. Kwa sasa, fikra na maombi yangu kwa Mungu ni kwa ajili ya majeruhi na familia zao´´.

Barack Obama amekwishakutana kwa mazungumzo na waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak na kiongozi wa upinzani wa kihafidhina Benjamin Netanyahu. Netanyahu ambae aliwahi kuwa waziri mkuu wa Israel, amesema Barack Obama ameahidi kutofanya chochote kinachoweza kuhatarisha usalama wa Israel. Wote hao wawili wamekubaliana kuzuwia Iran isimiliki silaha za kinyuklia. Baadae Barack Obama amepangiwa kukutana kwa mazungumzo na rais wa Israel Shimon Peres, waziri wa mambo ya kigeni Tzipi Livni na waziri mkuu Ehud Olmert ambae sasa anakabiliwa na kesi ya rushwa.

Barack Obama atalitembelea pia eneo la Wapalestina la Ukingo wa magharibi mwa mto Jordan kuzungumza na rais wa Palestina Mahmoud Abbas na waziri mkuu Salam Fayyad. Pia atafika katika mji wa Israel wa Sderot karibu na mpaka na eneo la Wapalestina la Gaza ambao hushambuliwa mara kwa mara kwa makombora kutoka eneo hilo la Gaza linalodhibitiwa na chama cha Hamas. John Mc Cain kutoka chama cha republikan na mshindani wa Barack Obama kwenye uchaguzi wa urais ujao nchini Marekani aliutembelea mji huo wa Sderot lakini hakufika kwenye Ukingo wa magharibi mwa mto Jordan. Barack Obama ambae ataendelea na ziara yake nchini Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, alisema ikiwa atachaguliwa kuwa rais wa Marekani, atashughulikia mpango wa kusaka amani kati ya Wayahudi na Wapalestina kwa lengo la kufikia mkataba wa amani ila alikiri kuwa haitokuwa kazi rahisi.

Alipokuwa bado nchini Jordan hapo jana, Barack Obama alisema atawasikiliza viongozi wa Israel na Palestina na kufanya kila juhudi kuusuluhisha mzozo kati ya Wayahudi na Wapalestina lakini kwamba hii haimanishi kwamba rais wa Marekani yeyote yule atakayechaguliwa, hatoweza kuleta suluhisho la mzozo huo peke yake.

 • Tarehe 23.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EiHb
 • Tarehe 23.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EiHb
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com