1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Askofu Desmond Tutu kuzikwa Januari Mosi

27 Desemba 2021

Mwanaharakati wa muda mrefu dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini Askofu Desmond Tutu aliyeaga dunia siku ya Jumapili atazikwa mnamo Januari Mosi katika mji wa kusini wa Cape Town.

https://p.dw.com/p/44qsH
Anglikanische Geistliche und Menschenrechtler Desmond Tutu verstorben
Picha: Paul Hawthorne/Getty Images

Wakfu wa Askofu Tutu aliyekuwa moja ya wanaharakati vinara wa kupinga ubaguzi wa rangi enzi ya utawala wa wazungu wachache nchini Afrika Kusini umesema mazishi ya kiongozi huyo wa kidini yatafanyika Januari Mosi baada ya wiki nzima ya maombolezo ya kitaifa, ibada ya kumuaga na mikusanyiko ya kutoa salamu za mwisho.

Taarifa iliyotolewa na wakfu huo imesema matayarisho tayari yanafanyika na ratiba kamili ya taratibu za mazishi ya mwanaharakati huyo aliyeheshimika duniani huenda itatolewa leo.

Tangu kutangazwa kwa kifo chake hapo siku ya Jumapili maelfu ya Waafrika Kusini wamekuwa wakijitokeza kwenye kanisa kuu la mtakatifu George mjini Cape Town kutoa salamu za heshima na rambirambi kwa askofu Desmond Tutu.

Wengi wanaweka mashada ya maua  chini ya picha ya Askofu Tutu iliyopo mbele ya jengo hilo la kanisa la kale mjini Cape Town.

Kifo chake chaleta kiwingu cha majonzi 

Südafrika Desmond Tutu und Egil Aarvik
Askofu Desmond Tutu akipokea Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 1984 Picha: Helmuth Lohmann/AP Photo/picture alliance

Kifo cha kiongozi huyo wa kidini ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel aliyotunukiwa mwaka 1984 kutokana na dhima yake katika kupinga ubaguzi wa rangi  nchini Afrika Kusini kimeleta huzuni kubwa sana kwa raia wa nchi hiyo na kwengineko duniani.

"Nimekuwa na majonzi tangu niliposikia kuwa amefariki. Ninamshukuru Mungu kwamba askofu huyu alikuwepo kwa ajili yetu" amesema mwombolezaji mmoja alipozungumza na shirika la habari la AFP mbele ya kanisa la mtakatifu George.

Wakati huo huo salamu za rambi rambi zimeendelea kumiminika kutoka kila pembe ya dunia zikimwelezea Askofu Desmond Tutu kama alama ya maadili nchini Afrika Kusini na mfano wa kuigwa kwa vizazi vya sasa na vinavyokuja.

Wakfu wake umemtaja kama mtu wa imani na vitendo aliyepinga vikali ubaguzi wa rangi, ukosefu wa haki, rushwa na ukandamizaji siyo tu ndani ya mipaka ya Afrika Kusini bali kote duniani.

Viongozi wa mataifa mengi wamlilia Askofu Tutu

Südafrika Desmond Tutu und Nelson Mandela
Marehemu Askofu Desmond Tutu akiteta jambo na hayati Nelson Mandela mwaka 1994 Picha: David Brauchli/AP Photo/picture alliance

Katika salamu zake za rambi rambi malkia Elizabeth wa Uingereza amesema kifo cha askofu Tutu ni pigo kwa raia wa Afrika Kusini na  Jumuiya nzima ya Madola ambako mchango wake uliheshimika sana.

Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani amesema mapambano ya Askofu Desmond Tutu dhidi ya ubaguzi wa rangi na mchango wake katika kulinda haki za binadamu, usawa na maridhiano vitakumbukwa na vitaenziwa daima.

Rais Joe Biden wa Marekani na mkewe Jill wameutaja urithi anaouacha Askofu Tutu kuwa utavuka mipaka na kudumu dahari dawamu.

Hisia kama hizo zimeelezwa pia na rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson na viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya.

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis amesema amehuzunishwa sana na kifo cha Askofu Tutu na kusifu kazi kubwa aliyoifanya katika kuhimiza usawa na maridhiano.