1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Askofu Desmond Tutu apumzishwa kwenye nyumba yake ya milele

Zainab Aziz Mhariri: Tatu Karema
1 Januari 2022

Askofu Mkuu wa Afrika Kusini Desmond Tutu aliyetoa mchango mkubwa katika harakati za kuutokomeza utawala wa kibaguzi amezikwa leo 01.01.2022.

https://p.dw.com/p/452uD
Südafrika Kapstadt Trauer um Desmond Tutu
Picha: AP/picture alliance

Maombolezo makubwa kwa ajili yake yalifanyika kwenye kanisa kuu la jiji la Cape Town, St George`s Cathedral ambapo amezikwa. Maombolezo yalianza kwa "Zaburi” na msafara wa makasisi waliochoma ubani na kuwasha mishumaa ndani ya Kanisa ambamo kwa miaka na miaka Askofu Mkuu Tutu alitumia mimbari kupambana na utawala wa kibaguzi wa makaburu.

Sanduku lililoubeba mwili wa marehemu Askofu Mkuu Desmond Tutu likiingizwa katika Kanisa kuu la jiji la Cape Town, St George`s Cathedral.
Sanduku lililoubeba mwili wa marehemu Askofu Mkuu Desmond Tutu likiingizwa katika Kanisa kuu la jiji la Cape Town, St George`s Cathedral.Picha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Watu nchini Afrika Kusini wamekuwa wanaomboleza kwa muda wa wiki nzima baada ya kifo cha askofu huyo aliekuwa na umri wa miaka  90.

Askofu mkuu wa Cantebury Justin Welby ambae ni kiongozi wa Kanisa Anglikana duniani amesema Tutu alileta mwangaza pale ambapo tulikuwamo katika kiza. Askofu mkuu Welby amesema kumsifu Askofu mkuu Tutu ni sawa na panya kumvisha tembo koja shingoni.

Askofu huyo Mkuu wa Cantebury amesema Afrika Kusini imetoa mfano wa viongozi mahiri, Nelson Mandela na Desmond Tutu waliotunukiwa nishani ya Amani ya Nobel. Welby ameeleza kuwa tofauti na wengine waliotunukiwa nishani hio, nyota ya Desmond Tutu  imeendelea kung'ara.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril RamaphosaPicha: Janine Schmitz/ photothek/picture alliance

Tutu hakutaka mazishi ya kifahari.Watoto na wajukuu zake waliyatekeleza maombi yake. Jeneza lake lilikuwa la kawaida kabisa. Maalfu ya watu miongoni mwao wale waliosafiri kutoka sehemu mbalimbali za nchi walitoa heshima zao mwisho.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema watu wa Afrika kusini wanamshukuru Askofu Mkuu Desmond  Tutu kwa yote aliyofanya kwa manufaa ya nchi yao: Pia amemshukuru Tutu kwa mchango mkubwa aliotoa katika harakati za kuung'oa utawala wa makaburu.Rais Ramaphosa amesema askofu Mkuu Tutu alikuwa mpiganaji wa mstari wa mbele katika harakati za kuleta uhuru, usawa na amani siyo tu nchini Afrika Kusini bali duniani kote.

Marehemu Askofu Mkuu Desmond Tutu July 22 mwaka 2010 alipotangaza kustaafu kwake.
Marehemu Askofu Mkuu Desmond Tutu July 22 mwaka 2010 alipotangaza kustaafu kwake.Picha: AP

Rais Ramaphosa amesema Tutu alikuwa mwadilifu. Kifo cha Askofu mkuu Tutu ni pigo kubwa kwa watu wa Afrika wanaomwita Askofu huyo Baba. Tutu alizaliwa mnamo mwaka 1931 magharibi mwa jiji la Johannesburg na kwanza alifanya kazi ya ualimu. Alitawazwa kuwa kasisi mnamo mwaka 1961.

Vyanzo:/DPA/AP