ANC yazindua kampeni ya uchaguzi wa bunge Afrika kusini | Matukio ya Afrika | DW | 13.01.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

ANC yazindua kampeni ya uchaguzi wa bunge Afrika kusini

Rais wa Afrika kusini Cyril Ramaphosa Jumamosi (12.01.2019)alizindua kampeni ya chama cha ANC ya uchaguzi wa bunge mwezi Mei, akikiri chama kufanya makosa hapo nyuma na kuahidi kurejesha taasisi za demokrasia.

Ramaphosa  aliwasilisha  manifesto yenye  kurasa  68 mbele  ya mamia  kwa  maelfu  ya  waungaji  mkono  chama  hicho  katika  mji wa  mashariki  wa  Durban, akizindua  miezi  minne  ya  kampeni.

Chama  cha  African National Congress  ANC, ambacho kimeitawala nchi  hiyo  tangu  kumalizika  kwa  utawala  wa  kibaguzi  miaka  25 iliyopita, kinatarajiwa  kushinda  uchaguzi  huo  licha  ya  kupungua kwa  uungwaji  mkono, migawanyiko  ya  ndani  pamoja  na  uchumi usio na  kasi  ya  ukuaji.

Südafrika ANC Parteitag (Getty Images/AFP/M. Safodien)

Waungaji mkono wa chama cha ANC kutoka Kwazulu Natal

Chama  cha  marehemu  Nelson  Mandela  kiliathirika  kwa  kupungua uungwaji  wake  mkono  chini  ya  urais  uliokumbwa  na  kashfa  tele wa  rais  Jacob zuma, ambaye  aliondolewa  Februari  mwaka  jana baada  ya  kuwapo  madarakani  kwa  miaka  tisa.

"tunapaswa  kukiri kwamba  makosa  yalifanyika," ramaphosa alisema, na  kuongeza: "Baada  ya  kipindi cha  shaka  na  hali  ya sintofahamu, tumewasili  katika  wakati wa  matumaini  na  ujenzi mpya.

"Uchaguzi  wa  mwaka  2019 unatoa fursa  ya  kurejesha  taasisi zetu  za  kidemokrasia  na  kuirejesha  nchi  yetu  katika  njia  ya mabadiliko, ukuaji  wa  uchumi  na  maendeleo."

Uchunguzi  wa  maoni

Katika  uchunguzi  wa  maoni  ya  wapiga  kura  uliofanyika  hivi karibuni  na  kundi  la  IPSOS umetabiri  kwamba  ANC inaweza kupata  kiasi  ya  asilimia  61 katika  uchaguzi  wa  bunge  la  taifa na  majimbo.

Südafrika ANC Parteitag Zuma und Ramaphosa (Getty Images/AFP/M. Safodien)

Rais wa zamani wa Afrika kusini Jacob Zuma (kushoto) na rais wa sasa Cyril Ramaphosa

Katika  kiwango  cha  bunge  la  taifa ,  hali  hiyo  itakuwa  sawa  na jinsi  chama  hicho  kilivyopata  katika  uchaguzi  wa  mwaka  2014, wakati  kilipopata  asilimia  62. Katika  bunge  la  Afrika  kusini, chama  hicho ambacho  kina  wingi  wa  viti pia  kina fursa  ya kumchagua  rais.

Ongezeko  hilo  la  utabiri  unatokana  na  kuteuliwa  kwa  rais ambaye  ni mwanamageuzi  mpenda  biashara  Cyril Ramaphosa baada  ya  wabunge  wa  ANC kumlazimisha  Zuma  kujiuzulu mnamo wakati  kashfa  za  rushwa  zikiongezeka.

Wanaharakati  ambao  walivalia nguo zenye  rangi  ya  chama  hicho za  manjano na  kijani  waliujaza uwanja  wa  mpira  wenye  uwezo wa  kuingiza  zaidi  ya  watu 85,000  katika  mji  huo  wa  pwani kwa ajili  ya  uzinduzi  huo na  walishangiria  kwa   nguvu  wakati  rais  wa zamani  Zuma , ambaye  anatoka  katika  eneo  hilo, alipojiunga  na kundi  la  wacheza ngoma katika  jukwaa.

Südafrika ANC Parteitag Ramaphosa und Nkosazana Dlamini-Zuma (picture-alliance/AP Photo/T. Hadebe)

Ramaphosa (kulia) na nksazana Dlamini-Zuma(kushoto) wakikumbatiana wakati wa kuwania kumrithi rais Zuma katika mkutano wa chama cha ANC

Katika tukio la  kupendeza  na  lililojaa  vifijo , dazeni  kadha  za wapanda  pikipiki wakipepea  bendera  ya  ANC , walizunguka  katika uwanja  huo , wakiendesha  pikipiki  zao  huku  wakishangiriwa  na kupigiwa  makofi.

Katika  mpambano  mkali  wa  ndani  wa  chama  hicho, Ramaphosa alishinda mpambano  wa  kuwania  madaraka  na  kumrithi Zuma, ambaye mgombea  aliyempendelea  alikuwa  mke  wake  wa  zamani.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Zainab Aziz