Amnesty yaitaka Tanzania ifanye uchunguzi madai ya mauaji | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.11.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Amnesty yaitaka Tanzania ifanye uchunguzi madai ya mauaji

Shirika la kimataifa la Amnesty International limesema serikali ya Tanzania inapaswa kufanya uchunguzi wa haraka, wa kina na ulio huru kuhusu madai ya mauaji dhidi ya wanasiasa wa upinzani na wafuasi.

Mkurugenzi Mkuu wa Amnesty International tawi la Mashariki na Kusini mwa Afrika, Deprose Muchena, amesema kumekuwa na ongezeko la ukiukaji wa haki za binaadamu baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa mwezi uliopita. Kwa mujibu wa mawakili wanaovitetea vyama vya upinzani, karibu viongozi 77 wa upinzani na wafuasi wao walikamatwa bila kufikishwa mahakamani tangu siku ya uchaguzi.

Amnesty International imesema kuukosoa uchaguzi ulivyofanyika sio uhalifu na kwa hivyo wote waliokamatwa bila kufunguliwa mashitaka wanapaswa kuachiwa huru mara moja na bila masharti yoyote. Muchena amesema viongozi wa Tanzania wanapaswa kuzilinda haki za Watanzania za uhuru wa kijielezea, kujumuika na kukusanyika kwa amani, kuliko kuzikiuka.

Sikiliza sauti 02:03

ACT- Wazalendo: Seif Sharif amekamatwa

Oktoba 31, kamishna wa polisi wa Zanzibar, Mohamed Haji Hassan, alithibitisha kwamba polisi inawashikilia watu 33, akiwemo naibu katibu mkuu wa chama cha upinzani ACT-Wazalendo, Nassor Mazrui. Mawakili wanaowawakilisha watuhumiwa wameripoti kuwa wengi wa watu waliokamatwa hawajafunguliwa rasmi mashtaka au hakuna ushahidi uliowasilishwa kuhusu madai ya ugaidi dhidi yao ambayo yanaonekana kuwa ya uwongo.

Bildkombo Tansania Wahlen | Präsident John Magufuli und Tundu Lissu

Rais Magufuli na mpinzani wake wa karibu Tundu Lissu

Aidha, huko huko visiwani Zanzibar, watu wengine 18 waliachiwa kutoka katika vizuizi na kutupwa kwenye maeneo mbalimbali majira ya asubuhi siku ya Novemba 13. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na baadhi ya waliokuwa wanashikiliwa na kuthibitishwa na mawakili wao.

Mawakili wa vyama vya upinzani wameliambia shirika hilo kwamba takriban watu 22 wameuawa na vikosi vya usalama kati ya tarehe ya uchaguzi na Novemba 11. Wanasiasa wa upinzani na mashirika ya kiraia wamevishutumu vikosi vya serikali kwa kutumia nguvu kupita kiasi, ikiwemo risasi za moto, kwa lengo la kuwatawanya waandamanaji. Viongozi lazima waanzishe uchunguzi kuhusu

Sikiliza sauti 04:03

Hatimaye Lissu aondoka Tanzania

mwenendo wa vikosi vya usalama.

Katika matukio mawili, Amnesty International iliwahoji ndugu za watu waliouawa, ambapo walikiri kwamba waathirika walikuwa na majeraha ya risasi. Aidha, wamesema ndugu zao waliouawa, hawakuwa wafuasi wa chama chochote kile cha kisiasa. Katika matukio mengine manne, shirika hilo limethibitisha kupitia mahojiano na watu walioshuhudia kwamba vikosi vya serikali vilihusika na mauaji. Kuna uwezekano kwamba idadi ya visa ikawa kubwa zaidi.

Kwa mujibu wa wanaharakati wa haki za binaadamu na mawakili wanaoviwakilisha vyama vya siasa, tangu kipindi cha uchaguzi zaidi ya watu 300 wamekamatwa nchini Tanzania, wengi wao wakiwa wameachiwa kwa dhamana na wengine bila kufunguliwa mashtaka. Miongoni mwa waliokamatwa na kuachiwa huru ni aliyekuwa mgombea wa urais wa chama cha upinzani Chadema, Tundu Lissu, mgombea urais wa ACT-Wazalendo visiwani Zanzibar, Seif Sharif Hamad na viongozi wengine wa upinzani,  Zitto Kabwe, Freeman Mbowe, Godbless Lema, Lazaro Nyalandu, Isaya Mwita, Boniface Jacob, Nassor Mazrui na Ayoub Bakari.

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com