Algeria kucheza na Brazil | Michezo | DW | 15.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Algeria kucheza na Brazil

Ikijiandaa kwa kombe lijalo la Afrika la mataifa, Algeria ina miadi na Brazil August 22.

Duru nyengine ya kuania tiketi za kombe la Ulaya la- champions League- inaendelea jioni hii baada ya Lazio Roma kutoka bao 1:1 na Dinamo Bucharest na Benefica Lisbon kuitimua Copenhagen 2:1.

FC Barcelona inaingia uwanjani jioni hii kwa changamoto na Bayern Munich kumuaga rasmi Mehmet Scholl na Algeria imemuita Hameur Bouazza, kutoka Fulham ,Uingereza ili kujiunga na kikosi chake kwa miadi na Brazil mjini Montpellier,Ufaransa, wiki ijayo.

Algeria inayojiwinda kwa changamoto za kombe la Afrika la Mataifa nchini Ghana 2008 ,ina miadi na Brazil kwa mpambano wa kirafiki huko Montpellier,Ufaransa August 22.Kwa changamoto hiyo,Algeria imemuita Hameur Boazza kujiunga na timu yao ya wachezaji 19 watakaoelekea Ufaransa.

Hamburg-mojawapo ya klabu zinazotamba katika Bundesliga, imekataa kuitikia hodi hodi za Valencia ya Spain kutaka kumuajiri nahodha wao mholanzi Rafael van der Vaart.Hamburg imeiarifu Valencia kuwa nahodha wao hataachiwa kuliacha mkono jahazi lake.

Leo katika uwanja wa Alllianz Arena,mjini Munich staid maarufu wa Bayern Munich na timu ya Taifa Mehmet Scholl,anaagwa rasmi.Mchezaji huyo wa kiungo ni maarufu wa kuchenga zake za ajabu na magoli yake maridadi.Akisimulia juu ya mafanikio yake Mehmet alisema:

“Mafanikio yangu makubwa ilikua katika Bayern Munich ambako katika kipindi cha miaka 15, nilivuka salama-usalimini nisimezwe na mapapa wakubwa wa klabu hiyo.”

Nae Kocha wa Bayern Munich Ottmar Hitzfeld akizungumza juu ya staid huyu alisema:

“Mehmet alikuwa staid mkubwa na mchawi wa dimba alielewa kuwatumbuiza mashabiki wake kwa werevu wake wa kusakata dimba.”

Alisema kocha wa Bayern Munich.Akieleza kwanini amestahiki mechi ya leo kati ya B.Munich na FC Barcelona kumuaga rasmi Mehmet Schöll,Ottmar hotzfeld alisema:

“Scholl ni mchezaji maarufu ambae amestahiki kuagwa vyema namna hii.”

Valencia iliocheza mara 2 finali ya kombe la klabu bingwa barani Ulaya imepiga hatua jana kukaribia kukata tiketi ya kucheza katika duru kamili ya champions League msimu huu.Valencia iliizaba jana Elfsborg ya Sweden kwa mabao 3:0.

Lazio Roma iliona wachezaji wake 2 wakitolewa nje ya chaki ya uwanja, mwishoe, iliweza kuokoa sare ya bao 1:1 nyumbani na Dinamo Bucharest ya Romania.

Benefica Lisbon ikailaza Copenhagen mabao 2:1 .Jioni hii ni zamu ya Liverpool ya Uingereza kukaribishwa na Toulouse huko Ufaransa wakati Ajax Amsterdam, ina miadi nyumbani na Slavia Prague ya Jamhuri ya Czech.

JS Kabylie ya Algeria ,inaongoza orodha ya timu 4 mabingwa wa zamani wa kombe la klabu bingwa barani Afrika wanaokabili kutimuliwa nje ya kinyan’ganyiro hicho mwishoni mwa wiki hii.

Kabylie inahitaji kutamba keshokutwa ijumaa huko nyumbani dhidi ya Al Ittihad ya Libya ama sihivyo iambiwe buriani katika kombe hili msimu huu.

Mabingwa Al Ahly wa Misri wanaongoza kundi B wakiwa na pointi 9 lakini wanaweza kupitwa na wenyeji wao Al Hilal ya sudan.

Mashindano ya kombe la dunia la rugby yatafanyika Ufaransa kuanzia Septemba 7 hadi oktoba 20 na Springbox –Afrika kusini inajiwinda kutamba.

 • Tarehe 15.08.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHbI
 • Tarehe 15.08.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHbI
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com