Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 06.12.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Wiki hii magazeti ya Ujerumani karibu yote yameandika juu ya kufariki dunia kwa kiongozi adhimu wa Afrika Kusini Nelson Mandela .Pia yameandika juu ya juhudi za Afrika za kuwalinda ndovu.

Hayati Nelson Mandela

Hayati Nelson Mandela

Gazeti la "die tageszeitung limesema Nelson Mandela aliikomboa Afrika Kusini kuondokana na mfumo wa kidhalimu wa ubaguzi wa rangi. Kutokana na busara yake watu wa Afrika Kusini wameutambua umuhimu wa kuishi pamoja kwa amani.Katika muhula wake wote wa urais Mandela alifanya juhudi kubwa za kuleta maridhiano katika nchi iliyokuwa inatawaliwa katika msingi wa rangi ya mtu.

Gazeti la "die tageszeitung" limeandika katika makala yake kwamba Afrika Kusini iliyokuwa inatambulikana kwa siasa za ubaguzi wa rangi na kuwatenganisha binadamu,iligeuka na kuwa jamii nyingine katika kipindi cha muda mfupi kutokana na juhudi za Mandela.

Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Gazeti la "die tageszeitung" wiki hii pia limeandika juu ya hali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na linasema watu wa nchi hiyo wanasubiri msaada. Ufaransa inawapeleka askari wake katika nchi hiyo. Nchi hiyo ambayo tayari imo katika mgogoro mkubwa imo katika hali mbaya sana. Gazeti la"die tageszeitung" linaarifu katika makala yake kwamba tokea alhamisi iliyopita Ufaransa inateremsha silaha nzito katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ikiwa pamoja na virafu.

Gazeti la"die tageszeitung " limewakariri viongozi nchini Ufaransa wakisema kwamba lengo la kuyapeleka majeshi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ni kuhakikisha ugavi wa misaada na kuwalinda wananchi wanaotishiwa na wapiganaji wa makundi mbaimbali.

Waislamu waandamwa Angola

Gazeti la "Süddeutsche"limetumia maneno makali kuilezea hali iliyotokea nchini Angola katika siku za hivi karibui Gazeti hilo limearifu juu ya kuandamwa kwa waislamu ambao ni jamii ya wachache nchini Angola.

Gazeti la "Südduetsche" linaarifu zaidi kwamba mtu ameweza kuziona picha zinazokumbusha usiku wa vigae nchini Ujerumani, usiku ambapo mafashisti walianza kuwaandamana wayahudi kwa kuwachomea moto nyumba na maduka yao. Watu wamepeleka picha katika mtandao zinazoonyesha msikiti uliopigwa moto na kugeuka jivu. Picha kama hizo zinapelekwa katika mitandao ya kijamii kuyaonyesha matukio hayo lakini zinaandamana na malalamiko dhidi ya serikali.

Gazeti la"Süddeutsche Zeitung" linatufahamisha kwamba picha hizo zimesababisha hasira katika sehemu kadhaa duniani.Kwa mfano katika Ukanda wa Gaza bendera ya Angola ilichomwa moto. Hata hivyo ilibainika baadae kwamba picha hizo hazikuwa sahihi kwani zilikuwa picha za zamani kutoka Nigeria. Gazeti la "Süddeutsche"linasema dini ya kiislamu haikupigwa marufuku nchini Angola lakini waislamu wanasumbuliwa .

Biashara haramu ya meno ya tembo na pembe za faru
Gazeti la "Der Tagesspiegel" linasema biashara haramu ya pembe za ndovu inastawi na nchi za Afrika sasa zinajaribu kutafuta njia ya kupambana na uhalifu huo. Gazeti hilo limeripoti juu ya mkutano wa kimataifa uliofanyika nchini Botswana kulijadili suala hilo.

Gazeti la "Der Tagespiegel" linafahamisha zaidi kwamba hakuna wiki hata moja inayopita bila ya kusikia kwamba maafisa wa idara za forodha wamezikamata tani za meno ya ndovu au pembe za faru barani Afrika.Kwa mujibu wa taarifa ya polisi ya kimataifa Interpol, biashara ya haramu ya pembe za ndovu imeongezeka mara mbili kati ya mwaka wa 2007 na mwaka huu.Thamani ya biashara hiyo inafikia kati ya Euro Bilioni 8 na13.

Gazeti la "Der Spiegel" limezikariri duru zinazosema kuwa kilo moja ya pembe ya kifaru inafikia dola alfu 40 na kila moja ya meno ya ndovu inafikia dola alfu 2 .Lakini gazeti la Der Spiegel linatilia maanani kwamba kwenye mkutano wa Botswana uliotishwa kulijadili suala la kuwalinda wanyama hao pori ni nchi 13 tu zilizohudhuria kati ya 37 zilizoalikwa. Gazeti la "Der Spiegel" pia limearifu kwamba ni Botswana na Zambia tu zilizotia saini azimio la mkutano.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Gakuba Daniel