Afrika Katika Magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 14.12.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika Katika Magazeti ya Ujerumani

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yamechapisha taarifa juu ya juhudi za kuutatua mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, na juu ya mapambano dhidi ya maradhi nchini Tanzania.

Waziri wa Ujerumani wa ushirikiano wa maendeleo Dirk Niebel

Waziri wa Ujerumani wa ushirikiano wa maendeleo Dirk Niebel

Gazeti la "die tageszeitung" limechapisha taarifa juu ya mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Gazeti hilo linaarifu kwamba baada ya waasi wa M23 kuondoka katika mji wa Goma, sasa wanafanya mazungumzo na serikali ya Kongo. Lakini wapiganaji wengi wa M23 wamekasirishwa na hatua hiyo ya kuondoka. Gazeti la "die tageszeitung "linafahamisha zaidi kuwa wapiganaji wa M23 wamo katika hatari ya kuvunjika moyo kufuatia hatua ya kuondoka katika mji wa Goma. Hali ya kutamauka iliweza kuonekana kwenye nyuso za wapiganaji hao.

Gazeti la "die tageszeitung" linaarifu kwamba baada ya miezi saba ya kuwapo misituni, wapiganaji wa M23 walishaanza kunogewa na maisha katika mji wa Goma. Gazeti hilo limeripoti kwamba hatua ya kuondoka katika mji huo imewakasirisha wapiganaji hao.

Gazeti la "Neues Deutschland" limeandika juu ya kapteni Amadou Haya Sanogo ambaye kwa kiasi kikubwa alisababisha sehemu ya kaskazini mwa Mali kutekwa na Waislamu wenye itikadi kali. Gazeti hilo limeandika kuwa Kapteni Sanogo amemwondoa madarakani Waziri Mkuu Cheick Modibo Diarra. Linakumbusha kwamba hii ni mara ya pili, mnamo mwaka huu kwa Kapteni huyo kujihusisha na tukio la kihistoria katika nchi yake. Mapema mwaka huu Kapteni Sanogo pamoja na maafisa wengine wa jeshi walimtimua kutoka madarakani Rais Amadou Toumani Toure. Nchi yake, sasa inahesabika kuwa tanuru kubwa la mgogoro barani Afrika kutokana na Waislamu wenye siasa kali kuitwaa na kuidhibiti sehemu ya kaskazini ambayo ni takriban theluthi moja ya Mali.

Gazeti la "Neues Deutschland" limeandika kwamba sasa Kapteni Sanogo anajaribu kuzituliza nchi za magharibi, kwani bila ya msaada wa nchi za magharibi nchi yake itakuwa na matatizo makubwa ya bajeti.

Ripota wa gazeti la "Frankfurter Allgemeine" anaarifu juu ya juhudi za Tanzania katika kupambana na maradhi ya kipindupindu na kichomi-yaani uvimbe wa mapafuni. Ripota huyo Peter Philipp Schmitt amearifu kuwa Mabalozi wa Italia na Marekani nchini Tanzania pamoja na mwakilishi wa wizara ya Ujerumani ya ushirikiano wa maendeleo walienda katika kitongoji cha Buguruni jijini Dar es Salaam na habari nzuri za kutangaza; mradi wa chanjo dhidi ya maradhi ya kipindupindu na kichomi. Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete alichukua hatua ya kwanza kumyunyizia mdomoni mtoto mmoja dawa ya chanjo dhidi ya magonjwa hayo hatari sana barani Afrika.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, maradhi hayo yanaua watoto wengi barani Afrika kuliko, maradhi ya Malaria, Ukimwi na Kifua Kikuu. Kuanzia mwezi wa Januari mwaka ujao Tanzania itakuwamo miongozi mwa nchi 24 ambazo tokea miaka mitatu iliyopita zimepokea msaada wa chanjo dhidi ya maradhi ya kichomi na itakuwa miongoni mwa nchi 12 itakayokuwa na mpango wa kutoa chanjo kwa watoto dhidi ya maradhi ya kichomi.

Waziri wa Ujerumani wa ushirikiano wa maendeleo, Dirk Niebel, ameitaka dunia isikubali njaa kuwa ni jaala kwa binadamu. Gazeti la "Berliner Zeitung" limemkariri Waziri Niebel akiyasema hayo kwenye mkutano uliofanyika mjini Berlin juu ya uhakika wa chakula duniani. Aliekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan pia alihudhuria mkutano huo Jumanne iliyopita. Gazeti la Berliner Zeitung limemkariri Kofi Annan akitoa mwito wa kukomesha mtindo wa kupora ardhi ya wakulima wadogo wadogo barani Afrika.

Mwandishi:Mtullya Abdu:Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Josephat Charo