Afisa Mafwele wa Tanzania marufuku kuingia Marekani
22 Mei 2026
Marekani imetangaza kumwekea vikwazo afisa mwandamizi wa polisi wa Tanzania Faustine Jackson Mafwele, ikimzuia kuingia nchini humo, kwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na jeshi la polisi.
Vikwazo hivyo vilivyotangazwa jana, vinafuatia uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka 2025, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alishinda muhula kamili kwa kupata asilimia 97 ya kura baada ya hatua kali za kubinya upinzani.
Katika taarifa yake, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema kuwa hatua ya kumwekea vikwazo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Faustine Jackson Mafwele inatokana na taarifa za kuaminika kuwa alihusika katika ukiukwaji wa haki za binadamu.
Mojawapo ya visa alivyovitaja ni kukamatwa, kuteswa na kuwafanyia unyanyasaji wa kingono wanaharakati Agather Atuhaire kutoka Uganda na Boniface Mwangi wa Kenya waliokwenda Tanzaniakufuatilia kesi iliyomkabili kiongozi wa upinzani Tundu Lissu.