ACT yamvua uwenyekiti Mghwira | Matukio ya Afrika | DW | 07.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

TANZANIA

ACT yamvua uwenyekiti Mghwira

Siku moja tu baada ya kuapishwa kuwa mkuu mpya wa mkoa wa Kilimanjaro, mwenyekiti wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo nchini Tanzania, Anna Mghwira amevuliwa uongozi wa chama chake kwa mgogoro wa maslahi.

Pamoja  na kumwondoa kwenye wadhifa wake huo, ACT-Wazalendo imempongeza Bi Mghwira kwa kuteuliwa kwake kikisema hatua hiyo inakisafishia njia chama hicho kuelekea katika uchaguzi ujao wa 2020.

Kwa mujibu wa kamati ya uongozi ya ACT, hatua ya kumwondoa mgombea wake huo wa urais mwaka 2015 kwenye nafasi ya uwenyekiti ilichukuliwa kwa kuzingatia katiba yake inayosema kuwa "kiongozi yoyote iwapo atashindwa kutekeleza vyema majukumu yake basi atakuwa ameondolewa kwenye wadhifa wake."

"Tumelazimika kuzungatia matakwa ya katiba yetu ili kutoa fursa kwa mgombea wake huyo wa zamani kutekeleza vyema majukumu yake mapya serikalini," alisema kaimu kiongozi mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Mwigamba alisema kwa ujumla chama chao kimeupokea kwa mikono miwili uteuzi wa Bi Mghwira, akidai kuwa unadhihirisha namna chama hicho kilivyokuwa na watu makini ambao wanaweza kuaminika na serikali iliyoko madarakani kuongoza.

Kaimu huyo aliongeza pia kuwa chama hicho kimefunguwa milango yake wazi kwa Rais John Magufuli kuteua viongozi wengine kwa kuwa asilimia kubwa ya vionogozi wake ni waadilifu na wenye moyo wa kizalendo, lakini kikitaka kwanza kiongozi huyo wa nchi kutafuta ushauri wa chama kabla ya uteuzi mwengine.

Bi Mghwira anakuwa mwanasiasa wa pili kutoka ACT kuteuliwa na Rais Magufuli katika serikali yake, akitanguliwa mshauri mkuu wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo, aliyeteuliwa kuwa katibu mkuu katika wizara inayoshughulikia maji na umwagiliaji hivi karibuni.

Hata hivyo, ACT si chama pekee cha upinzani ambacho viongozi wake wamefaidika na uteuzi wa Rais Magufuli, kwani hapo kabla alimteuwa kiongozi wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, kuwa mkuu wa parole.

Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com