1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ACT Wazalendo yajitenga na vurugu za kisiasa Zanzibar

Sudi Mnette
26 Machi 2019

Chama cha ACT Wazalendo nchini Tanzania kimepinga vikali tishio lililotolewa na msajili wa vyama vya siasa nchini humo la kutaka kukifuta chama hicho kwa maelezo kimekiuka sheria ya vyama vya siasa.

https://p.dw.com/p/3FfNt
Tansania Daressalam Zitto Kabwe
Picha: DW/S. Khamis

Kiongozi mkuu wa chama hicho Zitto Kabwe amekosoa vikali barua ya msajili huyo na kusisitiza kwamba hakuna kosa lolote ambalo chama chake kimefanya hadi kupewa tishio hilo. Akinukuu sehemu ya kifungu cha barua hiyo, Zitto amesema chama chake kimetuhumiwa kuchoma bendera za chama cha CUF tuhuma ambazo amesema hazina ukweli wowote. "Msajili alipatwa ajithibitishie, kwamba hao waliochoma kwamba ni wanachama wa ACT Wazalendo na nina uhakika hawezi kwenda mbele ya mahakama kwa kuwa sisi tunauhakika hao hawakuwa wanachama wetu"

 

Tansania Daressalam ACT Wazalendo
Bendera ya chama cha ACT WazalendoPicha: DW/S. Khamis

Kuhusu tuhuma kwamba baadhi ya wanachama wa chama hicho wamekuwa wakitamka maneno ya udini, Zitto ametupilia mbali shutuma hizo akisema matamshi ya Mungu mkubwa hayapaswi kuchukuliwa kama ni udini kwa vile ni sehemu ya maneno ambayo waumini wa aina yoyote wanaweza kuyatamka lakini wasifungamanishwe na imani za kidini.

Msajili wa vyama vya siasa ametoa muda wa siku 14 kwa chama hicho kujibu shutuma hizo na ametishia kukifutia usajili wake. Hata hivyo, Zitto mbali ya kusisitiza kuwa atatekeleza hilo lakini amesema chama chake kitaendelea na shughuli za kisiasa kama kawaida. Amesema chama chake kitafanya mawasiliano na jumuiya za kimataifa kuwasilisha kilio chao. Chama cha ACT Wazalendo hivi karibuni kilibadilisha upepo wa kisiasa nchini baada ya kumpokea mwanasiasa Maalimu Seif aliyekiaga chama chake cha awali cha CUF.

Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Daniel Gakuba