1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abbas apinga upatanishi wa Marekani kwa Mashariki ya Kati

Daniel Gakuba
28 Septemba 2018

Kiongozi wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas amesema Marekani haiwezi tena kuwa msuluhishi katika mzozo wa Mashariki ya Kati, kwa kuwa utawala wa Rais Donald Trump umedhihirisha kuegemea upande mmoja.

https://p.dw.com/p/35dLc
Mahmoud Abbas Rede vor der UN Generalversammlung
Mahmoud Abbas, Kiongozi wa Mamlaka ya WapalestinaPicha: picture-alliance/AP Photo/R. Drew

Kauli hiyo ya Rais Mahmoud Abbas ya kutupilia mbali uwezekano wa Marekani kuwa mpatanishi kati ya Israel na Wapalestina, ilitolewa siku moja baada ya Rais Donald Trump kudai katika hadhara hiyo hiyo kwamba anao mpango wa mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati, aliouita wa ''haki kabisa.''

Lakini Abbas alisema hatua ya Marekani ya kuzifunga ofisi za chama chake cha PLO mjini Washington, kuuhamishia ubalozi wake wa Israel mjini Jerusalem na kuzibana fedha zilizokuwa zikitolewa kama msaada kwa Wapalestina, vinaonyesha wazi inakoemea nchi hiyo.

Mbwa mwitu katika ngozi ya kondoo?

Abbas amesema ni unafiki mkubwa kwa utawala wa Marekani kuendelea kuzungumzia unachokiita 'mpango wa karne' wa amani, na kuongeza kuwa hakuna chochote ulichokibakisha utawala wa Trump cha kuwapa Wapalestina?

US-Präsident Trump spricht vor der Generalversammlung der Vereinten Nationen in New York
Rais wa Marekani Donald Trump, anasema anao mpango wa 'haki kabisa' kwa amani ya Mashariki ya KatiPicha: Reuters/C.Allegri

''Ni msaada wa kibinadamu? Kwa sababu, unapoiondoa Jerusalem, wakimbizi, usalama na vitu vyote kutoka  kwenye meza ya mazungumzo, kitu gani kimebaki wanachoweza kuwapa Wapalestina kama suluhisho la kisiasa?'' Aliuliza Abbas.

Kiongozi huyo wa Wapalestina mwenye umri wa miaka 82, alisema matendo ya utawala wa sasa wa Marekani, yamefuta ahadi zote zilizotolewa na viongozi waliotangulia, na kuhujumu uwezekano wa kuwepo kwa mataifa mawili ya Israel na Palestina. Mwezi Februari mwaka huu Abbas alizungumza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akataka uanzishwe upya mchakato wa amani kati ya Israel na Palestina, chini ya mpatanishi mwingine asiye Marekani.

Netanyahu aibuka na mchoro mpya

Benjamin Netanjahu Rede vor der UN Generalversammlung
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa IsraelPicha: Getty Images/AFP/T. A. Clary

Kabla ya Mahmoud Abbas, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alilihutubia pia baraza kuu la Umoja wa Mataifa, katika hotuba iliyoulenga hasa mpango wa nyuklia wa Iran. Kama kawaida yake ya kuzungumza akitumia vielelezo kuhusiana na mpango wa nyuklia wa Iran, jana alikuwa tena na kibao chenye michoro, ambayo alidai kinafichua kituo kingine cha Iran kilichoko mjini Tehran, chenye kuhifadhi zana zinazohusiana na uundaji wa silaha za nyuklia.

Netanyahu alisema ufichuzi wake huo unadhihirisha kwamba Iran bado ina azma ya kuunda silaha za nyuklia, licha ya makubaliano iliyoyatia saini na nchi sita zenye nguvu duniani mwaka 2015, ambapo iliahidi kupunguza shughuli zake ua kinyuklia ili iweze kuondolewa vikwazo. Marekani imekwishajitoa katika makubaliano hayo, chini ya utawala wa Rais Donald Trump.

Iran leo hii imezijibu shutuma hizo za Netanyahu, ikiziita za kipuuzi na zisizo na msingi. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Bahram Qassemi, amesema iran inaheshimu ukaguzi wa Shirika la Kimataifa la nishati ya Atomiki, ambalo amesema limethibitisha kwamba nchi hiyo inatekeleza majukumu yake.

Wakati huo huo ameishambulia Israel, akisema ni taifa pekee la Mashariki ya Kati lenye silaha haramu za nyuklia, akiitaka kuweka wazi  mpango wa silaha hizo ili ukaguliwe na taasisi za kimataifa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, afpe

Mhariri: Mohammed Khelef