Zuma asema hana hatia katika tuhuma za rushwa | Matukio ya Afrika | DW | 15.07.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Zuma awakabili waliosema kaiuza nchi

Zuma asema hana hatia katika tuhuma za rushwa

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma amekanusha tuhuma chungunzima zinazomuandama za kuhusika na vitendo vya rushwa na kuliambia jopo la uchunguzi yeye ni muhanga wa njama za kutaka kumuua.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma amekanusha tuhuma chungunzima zinazomuandama za kuhusika na vitendo vya rushwa na kuliambia jopo la uchunguzi kwamba alikuwa ni muhanga wa njama za kutaka kumuua. Zuma pia amewakosoa vikali wanaosema ameiuza nchi.

Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini alianza kujitetea mbele ya jopo hilo la uchunguzi kwa kusema hana hatia ya kosa lolote. Amekanusha madai ya kula rushwa yanayotolewa dhidi yake  akisema hayana ukweli wowote.

''Nimekuwa agenda ya gumzo katika nchi hii kwa zaidi ya muongo mmoja. nimetukanwa nikituhumiwa kuwa ni mfalme wa mafisadi.Nimepewa kila aina ya majina na sijawahi kujibu chochote.Kwanza kwasababu naamini ni muhimu kwamba watu waheshimiane na kwamba ni lazima mtu useme kile unachokijua kuhusu watu wengine na sio tu kusema vitu tusiivyoweza kuvithibitisha.''

Rais Zuma anasema kwa kipindi kirefu amekuwa muhanga wa kuandamwa na njama za kutaka kuuliwa ambapo ametowa tuhuma kwamna mashirika ya kijaasusi ya kigeni ambayo hakuyataja pamoja na wapelelezi wamekuwa wakishirikiana dhidi yake lakini akaongeza kusema kwamba alifanikiwa kunusurika majaribio ya kuuwawa.Kadhalika rais huyo wa zamani anasema familia yake imepitia hali ngumu kutokana na tuhuma zinazomuandama za rushwa akisema kwamba hawakuwa wakitaka kusikia kile alichokiita uwongo. Lakini pia mbele ya tume hiyo inayochunguza madai dhidi yake Zuma aliwakemea wale aliosema wamekuwa wakiendeleza kasumba za kudai kwamba ameiuza nchi.

''Je nilipiga mnada Temple Mountain au niliipiga mnada Johannesberg,sijui. Huyo bwana alikuwa amekaa hapahapa  nilipokaa mimi Zuma hivi sasa  aliposema ,Zuma ameiuza nchi,ndo sababu tukasema lazima aondoke.Lakini yote yalikuwa ni uongo.Hakuna kitu kama hicho.''

Zuma alikuwa rais wa Afrika Kusini kuanzia mwaka 2009 mpaka 2018 alipolazimishwa ajiuzulu na chama chake mwenyewe cha African National Congress ANC  kufuatia kuongezeka kwa ripoti zilizomtuhumu kwa ulaji rushwa.

Nafasi yake ilichukuliwa na aliyekuwa makamu wake wakati huyo Cyril Ramaphosa. Tume ya Zondo iliundwa kuchunguza tuhuma hizo na ombi la mahakama ni hatua muhimu ya  msukumo wa Ramaphosa wa kutaka kuondowa rushwa,suala ambalo ni ahadi aliyoitowa katika kampeini yake katika uchaguzi wa mwezi May ambapo chama chake kilipata ushindi wa asilimia 57.

Miongoni mwa tuhuma zinazochunguzwa ni madai ya familia ya kitajiri ya wafanyibiashara ya Guptas kuwa na ushawishi katika serikali ya Zuma wakati huo na kuifanya hadi kutowa maelekezo ya uteuzi wa baraza la mawaziri sambamba na kutoa maamuzi kuhusu nani alipaswa kupewa tenda za serikali.Mchakato wa kumuhoji Zuma katika kikao hicho huenda ukachukuwa wiki nzima  ingawa tayari rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 77 ameshasema yeye na familia yake hawajavunja sheria yoyote ya nchi.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo