1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma aanza kutumikia kifungo cha miezi 15 jela

Sylvia Mwehozi
8 Julai 2021

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma hatimaye ameanza kuitumikia adhabu ya kifungo cha miezi 15 jela baada ya kulala korokoroni usiku wa leo licha ya maandamano ya kupinga hukumu hiyo kutoka kwa wafuasi wake. 

https://p.dw.com/p/3wCn5
Südafrika | Jacob Zuma
Picha: Shiraaz Mohamed/AP Photo/picture alliance

Baada ya siku kadhaa za maigizo na chenga za kutaka kuikwepa adhabu hiyo, Zuma mwenye umri wa miaka 79 ameanza kutumikia kifungo cha miezi 15 jela baada ya kupelekwa leo katika gereza la EstCourt lililoko katika jimbo anakotoka la KwaZulu- Natal.

Zumaambaye ni mfungwa wa zamani wa utawala wa ubaguzi wa rangi, alizusha taharuki nchini humo baada ya kujaribu hatua za kisheria za kuepukana na adhabu hiyo, lakini kwa mara nyingine amejikuta mfungwa usiku wa jana. Hii ni mara ya kwanza kwa rais wa zamani kufungwa katika enzi za baada ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini. Singabakhe Nxumalo ni msemaji wa idara ya magereza.

"Zuma aliwasili tu baada ya saa saba usiku, unajua kuwa yeye ni rais wa zamani, ana kitengo cha ulinzi wa rais. Walimleta kwetu lakini sasa tunapaswa kuchukua jukumu na ninahitaji kuwahakikishia kuwa amezuiliwa katika ulinzi salama na pia tunapaswa kujibu mahitaji yake maalumu ikiwa kuna lolote limetambuliwa."

Hukumu hiyo iliyotolewa dhidi ya Zuma na mahakama ya katiba wiki iliyopita kwa kuwapuuza wachunguzi wanaofutilia madai ya ufisadi, pia iliiandika historia barani Afrika kwa kumfunga mkuu wa zamani wa nchi kwa kukataa kujibu mashitaka ya rushwa.

Wafuasi wa Zuma wakiwa nje ya makaazi yake huko Nkandla
Wafuasi wa Zuma wakiwa nje ya makaazi yake huko Nkandla Picha: Rogan Ward/REUTERS

Waafrika Kusini wengi wamesifu hukumu hiyo dhidi ya Zuma wakisema ilikuwa ni hatua moja kubwa katika kuimarisha utawala wa sheria nchini humo. Siku moja kabla, polisi walikuwa wameonya kwamba wangemkamata Zuma baada ya muda wa mwisho ambao ulikuwa ni usiku wa jana ili kutekeleza sheria, isipokuwa tu kama mahakama ingeagiza vinginevyo.

Dakika chache kabla ya muda huo kumalizika, taasisi yake iliandika kupitia ukurasa wa Twitter kwamba Zuma "ameamua kutii agizo la kifungo" na amejisalimisha mwenyewe kwenye jela ya EstCourt.

Zuma aliwahi kutumikia kifungo cha miaka 10 jela katika gereza la Roben island kutokana na ushiriki wake kwenye harakati za ukombozi dhidi ya utawala wa mfumo wa kibaguzi. Jumatatu ijayo mahakama ya katiba itazingatia shauri alilowasilisha Zuma la kufutwa kwa adhabu ya kifungo gerezani. Kupitia mawakili wake, Zuma ameieleza mahakama kwamba adhabu ya kifungo cha gerezani inahatarisha maisha yake kwa kuzingatia afya yake ambayo ni dhaifu.

Zuma anatuhumiwa kujihusisha na masuala ya hongo miaka 20 iliyopita5. Pia anakabiliwa na mashitaka 16 ya ulaghai, rushwa na ulanguzi unaohusiana na ununuzi wa ndege za kivita, boti za doria na vifaa vya kijeshi kutoka kampuni tano za silaha za Ulaya kwa randi bilioni 30 sawa na dola bilioni 5 za kimarekani.

Vyanzo: AFP/DPA