1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Steinmeier nchini Israel magazetini

Josephat Charo
10 Mei 2017

Mada zilizohanikiza katika magazeti ya Ujerumani leo ni ziara ya rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeir nchini Israel na kashfa inayolikabili jeshi la Ujerumani, Bundeswehr.

https://p.dw.com/p/2cjTr
Israel Nahost Frank-Walter Steinmeier bei Amir Peretz
Picha: AP

Kuhusu ziara ya Steinmeier nchini Israel, gazeti la Rhein Zeitung linaandika: Licha ya rais wa Marekani Donald Trump kuahidi kuupatia ufumbuzi mgogoro wa mashariki ya kati, hakuna matumaini yoyote ya kupatikana ufanisi katika siku zijazo. Ni jitihada mpya tu ya rais mpya wa Marekani.

Ni jambo la kushangaza na lisiloingia akilini kwamba Trump ndiye anayewekewa matumaini ya kuutanzua mzozo wa Mashariki ya Kati. Waisraeli na Wapalestina wote wanamtegemea yeye. Hiyo ni kama kupanga kuvunjika moyo. Na hata viongozi wa Ulaya katika mgogoro huu hawamshubiri mtu yeyote. Ndio maana ilikuwa sahihi kwa rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeir kutochukua jukumu kubwa la mpatanishi. Kwa kulitembelea kaburi la kiongozi wa zamani wa Wapalestina, Yasser Arafat, Steinmeier alitoa ishara ya kuunga mkono suluhisho la mataifa mawili. Hilo ndilo jambo dogo aliloweza kulifanya.

Gazeti la Südwest-Presse la mjini Ulm limeandika kuhusu uhusiano kati ya Ujerumani na Israel. Mhariri anasema rais Steinmeier alifaulu kulikabili wimbi la siasa za Israel bila kuligusia moja kwa moja suala la waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel ambaye waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikataa kukutana naye baada ya Gabriel kukutana na kundi linalopinga kukaliwa ardhi ya Wapalestina. Mhariri aidha anasema ziara ya Steinmeier ilikuwa na tija kwa sababu alionya hadharani kwamba kuwazuia viongozi kutoa maoni yao hakusaidia ufahamu wa mambo.

Kashfa katika jeshi la Ujerumani

Maafisa wa Ujerumani jana walimtia mbaroni mwanajeshi wa pili kwa kuhusika na njama ya kufanya shambulio la kigaidi. Kuhusu kashfa hii katika jeshi la Ujeruamani Bundeswehr, gazeti la Leipziger Volkszeitung linasema bado inasubiriwa kuona mtandao wa kigaidi una upana gani. Nani mwanachama, nani alishikirikiana na nani na kivipi.

Mhariri wa gazeti la Leipziger Volkszeitung anasema imedokezwa kuwepo kwa maghala ya siri ya silaha. Iliwezekana vipi silaha kupotea? na zilikwenda wapi? Nani anayeficha siri hapa? Mhariri anasema suala hili halishughulikiwi na uzito unaotakiwa. Waziri anayehusika Ursula von der Leyen hajajitetea kuhusu suala hili lakini amekubali kuikabili changamoto bila kuzungumzia ari ya wanajeshi inayoeleweka vibaya. Amelikemea na kutaka yaanzishwe tena maadili ya kidemokrasia. Na hili mhariri anasema ni jambo la dharura.

Türkische Soldaten erhalten erstmals Asyl
Picha: picture alliance/AA/H. M. Sahin

Ujerumani yawapa hifadhi maafisa wa jeshi la Uturuki

Mada nyingine iliyozingatiwa na wahariri hii leo ni hatua ya Ujerumani kuwapa hifadhi maafisa wa jeshi la Uturuki. Gazeti la Badische Zeitung la mjini Freiburg linasema kama mtu anataka kuwa mkweli, uhusiano na Uturuki kwa muda mrefu umekabiliwa na changamoto nyingi za kisiasa. Mazungumzo kuhusu Uturuki kutaka kujiunga na Umoja wa Ulaya, yamekuwa yakiendelea kwa muda mrefu.

Mhariri anasema kila mtu anafahamu mazungumzo haya hayataleta tija. Ujerumani imewasaidia wakimbizi kutoka Uturuki, wengi wakiwa Wakurdi wanaopata usalama, hata maombi yao ya kupewa hifadhi yanapokataliwa. Kwa mara ya kwanza wanajeshi wa Uturuki pia wametambuliwa kama wakimbizi na kansela Angela Merkel amesema Waturuki hawataruhusiwa kushiriki kura ya maoni kuhusu kuirejesha tena adhabu ya kifo nchini Uturuki. Mhariri anasema Uturuki inafanya itakavyo. Ujerumani inasimamia maadili mengine.

Mwandishi:Josephat Charo/Inlandspresse

Mhariri:Iddi Sessanga