Ziara ya kansela Angela Merkel Ugiriki | Magazetini | DW | 10.10.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Ziara ya kansela Angela Merkel Ugiriki

Ziara ya kansela Merkel nchini Ugiriki,sheria za uhamiaji kupunguzwa makali na maonyesho ya kimataifa ya vita mjini Frankfurt ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani .

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel(kushoto) na waziri mkuu wa Ugiriki Antonis Samaras

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel(kushoto) na waziri mkuu wa Ugiriki Antonis Samaras

Tuanzie lakini Ugiriki ambako ziara ya kansela wa Ujerumani iligubikwa na maandamano ya wanaopinga hatua za kufunga mkaja zinazolazimishwa na Umoja wa Ulaya,shirika la fedha la kimataifa na benki kuu ya Ulaya. Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" linaandika:

Vyovyote vile mgogoro wa sarafu ya Euro na mzozo wa Ugiriki utakavyokuwa,mkutano kati ya kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa Ugiriki Antonis Samaras kamwe hautasahauliwa.Nembo ya tawala wa zamani wa wanazi ,idadi kubwa kupita kiasi ya vikosi vya usalama na mikururo ya watu walioandamana kwa amani:Yote hayo hayajawahi kushuhudiwa mkuu wa serikali ya Ujerumani anapofanya ziara nchi za nje.Samaras na Merkel wanastahiki hishma na cheo .Msimamo wao ndio unaobainisha mshikamano wao.Tukiyatenga maandamano,mtu anaweza kusema kuna kila sababu ya kuamini kwamba mkutano wao umetekeleza lengo la suluhu lililowekwa.Ukweli wa mambo lakini umesalia vile vile.

Gazeti la "Neue Westfälische" linahisi pia licha ya ziara hiyo,mambo yako vile vile.Gazeti linaendelea kuandika:

Ziara ya kansela wa Ujerumani nchini Ugiriki haijasaidia kumaliza mgogoro mkubwa unaowakaba wagiriki.Bado nchi yao inakumbwa na kitisho cha kufilisika na wala hakuna anaeweza kudhamini kuwepo kwao milele katika kanda ya Euro.Lakini Angela Merkel amekwenda Ugiriki wakati muwafak na kuwapelekea risala inayofaa.Ingawa alichobeba,Euro milioni 30 ni haba,lakini siasa ina uzito zaidi kuliko fedha.

Protestmarsch für Flüchtlinge und Asylbewerber von Würzburg nach Berlin

Maaandamano kudai kuboershwa hali ya wakimbizi

Mada yetu ya pili magazetini inahusu sheria inayowazuwia wanaomba kinga ya ukimbizi kuranda randa.Gazeti la "Berliner Zeitung" linaandika:

Katika jimbo la kusini la Bavaria,wenyewe wanasema,hakuna njia nyengine.Wakimbizi wanaweza kutoroka wakiruhusiwa kwenda kokote kule wakutakako humu nchini.Fikra hizo haziingii akilini.Wakimbizi hawafikirii kuishi kinyume na sheria.Wengi wao wanataraji wapate fursa ya kuishi maisha ya kawaida tu.Na atakaefikiria kutoroka,kibali kinachomlazimisha kuishi katika eneo moja tu hakitamzuwia kufanya hivyo.Baadhi ya majimbo ya Ujerumani yameshautambua ukweli huo na kuregeza makali ya sheria hizo.Wakati umewadia wa kuziibatilisha kabisa.

Buchmesse Frankfurt 2012

Maonyesho ya kimataifa ya vitabu mjini Frankfurt

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu kufunguliwa maonyesho ya kimataifa ya vitabu mjini Frankfurt na changamoto inayowakabili wachapishaji na vitabu katika enzi hizi za mtandao na digitali.Gazeti la "Der Tagesspigel" linaandika:

Kitabu,kama tunavyokijua tangu karne kadhaa zilizopita,hakijatoweka licha ya kuibuka enzi za digitali.Kwasababu vyombo vya kusomea vya elektronik na vitabu vijulikanavyo kama E-Books havitoi tija ya kutosha hasa mtu anapotaka kuvisoma vitabu vya aina hiyo.Bila ya kuzitaja shida zinazojitokeza na ambazo zimeandaliwa makusudi na makampuni mfano wa Apple,Sony au Amazon.Hata hivyo lakini kitabu tulichokua tukikijua hadi sasa kimo mashakani.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman