1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yuko wapi Mwandishi Habari Azory Gwanda?

Admin.WagnerD4 Aprili 2019

Kamati ya kimataifa ya kuwalinda waandishi wa habari CPJ imezindua kampeni kubwa kuhusu kisa cha kupotea mwandishi habari wa nchini Tanzania Azory Gwanda ambaye kesho Ijumaa anatimiza siku 500 tangu alipotoweka.

https://p.dw.com/p/3GDyr
dw freedom Azory Gwanda

Kulingana na taarifa iliyotolewa leo na kamati hiyo mjini New York, kampeni iliyozinduliwa imepewa jina la Yuko wapi Azory mwandishi wa Habari wa kujitegemea kutoka Tanzania ambaye alitoweka kiasi mwaka mmoja na nusu uliopita katika mazingira ya kutatanisha.

CPJ imesema kampeni ya Yuko wapi Azory inalenga kujenga uelewa kuhusu mwandishi huyo wa habari na kutoa shinikizo kwa mamlaka nchini Tanzania kuanzisha uchunguzi wa kuaminika na kutoa taarifa bayana kuhusiana na kisa cha kupotea kwake.

Mratibu wa kamati ya CPJ kanda ya Afrika, Angela Quintal amesema kupitia kampeni hiyo itakayohusisha pia kupaza sauti kupitia mitandao ya kijamii CPJ inataka kesi ya Gwanda ipewe kipaumbele na mamlaka za Tanzania na kupata majibu yanayokubalika kuhusu kile kilichomsibu.

Hakuna majibu kuhusu alipo Azory

Azory Gwanda - Journalist (Mwananchi Communications Limited (MCL) in Tanzania
Picha: Privat

Hadi sasa hakuna maelezo yoyote kutoka vyombo vya usalama nchini Tanzania kuhusu alipo mwandishi huyo na kile kilichompata.

Tangu kupotea kwake polisi ya Tanzania imesema mara kadhaa kuwa bado inafanya uchunguzi.

Azory Gwanda ambaye alikuwa akifanya kazi na kampuni ya magazeti ya Mwananchi nchini Tanzania alitoweka tarehe 21 Novemba 2017.

Gwanda alikuwa akiishi na kuripoti kutoka mji mdogo uitwao Kibiti, ambao upo kiasi kilomita 130 kusini mwa mji wa kibiashara wa Dar es Salaam.

Bwana Gwanda ni mmoja wa waandishi wa kwanza kabisa kuripoti kwa kina juu ya mfululizo wa mauwaji yaliyokuwa yakitekelezwa na watu wasiojulikana yaliyowalenga polisi na viongozi wa mji huo.

Kupotea kwa mwandishi huyo kunahushishwa na kufuatilia kwake yaliyokuwa yakiendelea hasa madai kwamba vyombo vya usalama vilikuwa vikitekeleza vitendo vya unyanyasaji dhidi ya raia katika juhudi za kudhibiti matukio ya mauaji kwenye mji wa Kibiti na wilaya jirani.

Kisa cha Azory ni kitisho kwa uhuru wa waandishi

LOGO CPJ

Mke wa Azory, Anna Pinoni aliviambia vyombo vya habari kuwa siku ya tukio watu wanne wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser walimchukua Gwanda kutoka katikati ya mji huo, kisha kwenda naye nyumbani kabla ya baadae kutoweka hadi sasa.

Kampeni kadhaa zimeanzishwa kutaka maelezo juu ya kupotea kwa Azory, lakini hakuna majibu hadi sasa.

CPJ ambayo ni kamati huru, isiyojiendesha kwa faida na inayofanya kazi za kulinda uhuru wa waandishi habari duniani kote imesisitiza kuwa mkasa wa kupotea kwa Azory Gwanda umesababaisha hofu miongoni mwa waandishi habari nchini Tanzania.

Kupotea kwa Azory kunatokea wakati ambapo malalamiko ya kuzorota kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania yakiongezeka, ikiwa ni pamoja na maagizo ya serikali kuvifungia baadhi ya vyombo vya habari, kuvitoza faini, kutungwa kanuni zenye vizuizi na kukamatwa hovyo waandishi wa habari.

Mwandishi: Rashid Chilumba

Mhariri: Grace Patricia Kabogo