Yemen Yafanya Uchaguzi wa Rais | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.02.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Yemen Yafanya Uchaguzi wa Rais

Wananchi wa Yemen wanapiga kura leo kumchagua rais mpya, kuchukua nafasi ya Ali Abdullah Saleh ambaye ameachia madaraka chini ya mkataba wa kumaliza machafuko. Kulikuwa na uitikiaji mkubwa licha ya visa vya fujo.

Shabiki akibebe picha ya mgombea Abd-Rabbu Hadi

Shabiki akibebe picha ya mgombea Abd-Rabbu Hadi

Makamu Rais Abd-Rabbu Mansour Hadi ndie mgombea pekee katika uchaguzi huu ambao unatarajiwa kuandika ukurasa mpya katika siasa za Yemen, baada ya utawala wa miaka 33 wa Rais Ali Abdoullah Saleh. Rais Saleh ambaye kwa wakati huu yuko Marekani atakuwa kiongozi wa nne kuondolewa madarakani, baada ya upepo wa mageuzi kuanza kuvuma katika ulimwengu wa Kiarabu. Upepo huo tayari umebadilisha uongozi katika nchi za Tunisia, Misri na Libya.

Makamu Rais Abd-Rabbu Mansour Hadi ndie mgombea pekee

Makamu Rais Abd-Rabbu Mansour Hadi ndie mgombea pekee

Leo asubuhi kulikuwa na mistari mirefu ya wapiga kura mbele ya vituo vya uchaguzi katika mji mkuu Sanaa, huku ulinzi ukiwa umeimarishwa. Jana, bomu liliripuka ndani ya kituo cha kupigia kura katika mji wa kusini wa Eden. Leo hii pia kumeripotiwa machafuko katika mji mwingine wa kusini wa Makalla, ambamo wanamgambo wenye silaha wamekivamia kituo cha uchaguzi na kumuua askari mmoja.

Harakati za kutetea uhuru na haki zitaendelea

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Tawakul Karman amesema uchaguzi huu ni kama tangazo rasmi kuuaga utawala wa Rais Ali Abdullah Saleh na kuanza enzi mpya, na kuongeza kuwa wataendelea na mapambano.

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Tawakul Karman

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Tawakul Karman

''Hatuwezi kukaa kimya wakati nchi yetu ikielekezwa pabaya. Tutaendeleza mapambano kuhakikisha tunapata haki yetu ya kujieleza kwa uhuru, tutapinga ufisadi, na tutatetea uhuru wetu na haki zetu.'' Amesema Karman.

Kujitokeza kwa idadi kubwa ya wapiga kura ni jambo muhimu ili kuhalalisha madaraka ya Abd-Rabbu Mansour Hadi, yaliyokabidhiwa kwake kupitia mkataba wa amani uliodhaminiwa na nchi za Ghuba. Miongoni mwa majukumu yenye kipaumbele yanayomsubiri ni kusimamia kuandikwa kwa katiba mpya, na kulifanyia mageuzi jeshi ambalo linadhibitiwa na ndugu wa Rais Ali Abdullah Saleh.

Matunda ya vuguvugu la mageuzi

Mmoja wa wapiga kura, Ziadi al Qitwi aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba kupitia uchaguzi huu, wana imani ya kumaliza utawala wa kiimla wa Rais Ali Abdullah Saleh, na pia ushawishi wa watu kutoka familia yake. Amesema hatua hii na matunda mema, baada ya mapinduzi ya mwaka mzima.

Rais anaeondoka madarakani, Ali Abdullah Saleh

Rais anaeondoka madarakani, Ali Abdullah Saleh

Uchaguzi wa leo unaungwa mkono na Marekani, pamoja na Saudi Arabia, jirani wa Yemen mwenye ushawishi mkubwa kikanda na ambayo ilidhamini mazungumzo ya amani yalisainiwa mwezi Novemba mwaka jana.

Hata hivyo, uchaguzi huu unafanyika kukiwa na changamoto kubwa ambazo bado hazijapatiwa ufumbuzi. Makabiliano ya kijeshi yanaendela baina ya majenerali wenye uhusiano na Rais Ali Abdullah Saleh na wengine watiifu kwa viongozi wa makabila. Kuna pia mgawanyiko baina ya kusini na kaskazini, huku wanamgambo wa kiislamu kutoka maeneo ya kusini na wenye mafungamano na al-Qaida wakitaka kujitenga.

Wito wa umoja kuepusha msambaratiko

Katika hotuba yake kwenye mkesha wa uchaguzi, mgombea wa pekee Abd Rabbu Mansour Hadi amewaomba wananchi wa Yemen kuweka kando tofauti zao, ili nchi hiyo isije kusambaratishwa na vita vya wenyewe kama ilivyotokea Somalia.

Uchaguzi wa leo unachukuliwa na wachambuzi kama nafasi muhimu ya kujenga upya nchi hiyo, ambayo kwa takribani mwaka mmoja uliopita ilikumbwa na ghasia zilizotishia kuitumbukiza katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/Reuters

Mhariri:Abdul-Rahman, Mohammed

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com