1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa zamani DRC aliehamia upinzani akutwa amekufa

Jean Noël Ba-Mweze
14 Julai 2023

Chama cha upinzani cha Ensemble pour la République kinachoongozwa na Moise Katumbi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kimetaka ufanyike uchunguzi huru baada ya kuuawa mbunge wake, Chérubin Okende siku ya Alhamisi

https://p.dw.com/p/4TvEy
Demokratische Republik Kongo Kinshasa | Cherubin Okende
Marehemu Cherubin Okende akishiriki maandamano ya upinzani mjini Kinshasa, Machi 11, 2023. Okende alipigwa risasi mjini Kinshasa, na mwili wake kugundulika Alhamisi, Julai 13, 2023.Picha: Samy Ntumba Shambuyi/AP/picture alliance

Cherubin Okende alikuwa mwanachama wa chama cha Moise Katumbi, kiongozi maarufu wa upinzani ambaye anatazamiwa kuwania uchaguzi wa rais katika taifa hilo la Afrika ya Kati hapo Desemba.

Baada ya kupatikana mwili wake serikali iliiagiza haraka mahakama kuanzisha uchunguzi ili kubaini ukweli zaidi kuhusu mauaji hayo. Mshukiwa wa kwanza akiwa ni mlinzi wake tayari amekamatwa kwa uchunguzi na sasa yupo korokoroni akihojiwa.

Soma pia: Upinzani DR Kongo wamtaka Tshisekedi kuacha kuwachokoza

Afisa kutoka timu ya Katumbi aliliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, kwamba Okendi, 61, alitoweka siku ya Jumatano baada ya kusafiri kwa ajili ya miadi katika mahakama ya katiba mjini Kinshasa.

Moise Katumbi
Kiongozi wa chama cha Ensemble pour la République, Moise Katumbu anatazamiwa kugombea urais katika uchaguzi wa Desemba 2023.Picha: Nicolas Maeterlinck/BELGA/dpa/picture alliance

Mwili wake uliojaa matundu ya risasi ulikutwa Alhamisi asubuhi katika gari lake kwenye mmoja barabara za mji mkuu, aliongeza afisa huyo.

Mahakama yakana kutekwa mlangoni pake

Dieudonné Kamuleta ambae ni mwenyekiti wa mahakama ya Kikatiba aliwaelezea waandishi wa habarisiku ya Alhamisi kwamba matokeo ya uchunguzi ndiyo yatakayothibitisha kama marehemu Okende alitekwa nyara katika eneo la Mahakama ya Kikatiba kama chama chake kinavyodai au la.

Soma pia: DRC: Mawaziri watatu wajiuzulu

"Sisi tunayo barua yake ya kusema kwamba hangeweza kuja. Halafu ikiwa alikuja na kukaa nje, wewe na mimi hatuwezi kujua. Lakini tunashikilia kile ambacho ni rasmi," alisema Kamuleta na kufafanua kuwa marehemu alisema hangeweza kuja Alhamisi bali Ijumaa.

Mauaji ya Okende yamejiri zaidi ya mwezi mmoja baada ya kukamatwa kwa Salomon Idi Kalonda, ambaye anatuhumiwa kuwasiliana na waasi wa M23 pamoja na maafisa wa Rwanda ili kuupindua utawala wa Rais Felix Tshisekedi.

DRC Afrika Treffen  Felix Tshisekedi
Rais wa DRC, Felix Tshisekedi.Picha: presidential press service of the DRC

Mshauri wa Katumbi atuhumiwa kutaka kumpindua Tshisekedi

MONUSCO yaombwa kusaidia uchunguzi huru

Chama chake cha Ensemble pour la République, kimeeleza kusikitishwa na mauaji ya msemaji wake na kinataka kufanyika uchunguzi huru ukishirikisha pia tume ya Umoja wa Mataifa nchini Kongo, MONUSCO.

Soma pia: Martin Fayulu awataka Bemba na Katumbi kuchukuwa maamuzi

"Chérubin Okende alikuwa katika eneo ambapo moyo wa Jamhuri unadunda kila siku. Tunatoa wito wa uchunguzi huru na tunatumai MONUSCO, ambayo ina vyombo vyote vya uchunguzi itahusishwa ili ukweli udhihirike na hivyo wauaji pamoja na wafadhili wa uhalifu huo kutambuliwa pia kuadhibiwa", alisema Olivier Kamitatu, msemaji wa Moise Katumbi.

Chérubin Okende alikuwa waziri katika serikali inayoongozwa na Jean-Michel Sama Lukonde kabla ya kujiuzulu ili kubaki mwaminifu kwa kiongozi wake Moïse Katumbi ambaye aliachana na Rais Tshisekedi.

Hali imekuwa tete miezi mitano tu kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba, ambapo Moïse Katumbi ni mmoja wa wagombea urais wanaotazamiwa kushindana dhidi ya rais Tshisekedi.