1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC: Mawaziri watatu wajiuzulu

Jean Noël Ba-Mweze
29 Desemba 2022

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mawaziri watatu wa serikali kuu na mmoja wa serikali ya mkoa, wote wanachama wa Ensemble pour la République, cha Moise Katumbi, wamejiuzulu.

https://p.dw.com/p/4LWf5
Felix Tshisekedi
Picha: Boniface Muthoni/SOPA Images/ZUMA/picture alliance

Mawaziri hao watatu waliojiuzulu ni Christian Mwando, waziri wa mipango, Chérubin Okende, waziri wa uchukuzi na mawasiliano pia Véronique Kilumba, naibu waziri wa afya, pamoja na Christian Momat, waziri wa mipango mkoani Haut-Katanga.

Wanachama hao wanne wa Ensemble pour la République wamejiuzulu siku chache tu baada ya kiongozi wa chama chao Moses Katumbi, kuamua kujitenga na muungano wa vyama vinavyomuunga mkono rais Félix Tshisekedi, na kutangaza rasmi kuwania urais katika uchaguzi unaotarajiwa nchini DRC mnamo Disemba 2023.

Muda mfupi kabla ya kufunguliwa Baraza la Mawaziri jana Jumatano, Rais Tshisekedi aliwapokea mawaziri watano kati ya sita wa serikali kutoka chama hicho, mmoja wa hao sita, Muhindo Nzangi ambae ni Waziri wa Elimu na vyuo vikuu ambaye hayupo nchini kwa sababu za kazi. Mawaziri Christian Mwando, Chérubin Okende na Naibu Waziri Véronique Kilumba walionyesha mshikamano na uaminifu wao kwa chama chao.

Moise Katumbi
Kiongozi wa chama cha Ensemble Moise Katumbi ametangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi ujao, 2023.Picha: Nicolas Maeterlinck/BELGA/dpa/picture alliance

Christian Mwando ambaye ni waziri wa zamani wa mipango alisema "Naamini wapo wengine wengi watakaojiuzulu kutoka taasisi. Ni chaguo la uaminifu na la kisiasa kwa sababu tunapaswa kuwa na msimamo wa kisiasa na sio kuendelea kutekeleza siasa za tumbo. Uaminifu ni muhimu kwa Wakongo na ninaamini kuwa nchi yetu inauhitaji."

Upande wa muungano wa vyama vinavyomuunga mkono rais Félix Tshisekedi, wameelezea kujiuzulu kwa viongozi hao wafuasi wa Moses Katumbi kuwa hakuna maana au tukio lolote.

Meshack Mandefu, mmoja wa viongozi wa muungano huo anawataja mawaziri wafuasi Katumbi kuwa wanafiki, akisema "Kujiuzulu huko hakuna maana au tukio kwani tulijua kwamba mawaziri wafuasi wa Katumbi walikuwa wakifanya unafiki. Muungano wetu unaundwa na viongozi kadhaa wa vyama vikuu na hivyo, kujiuzulu huko hakuwezi kutudhoofisha hata. Ikibidi leo kuchunguza serikali ya Sama Lukonde, Moses Katumbi pia alishiriki."

Huko viongozi wengine watatu wa chama cha Katumbi wakiwemo Christophe Lutundula, Naibu Waziri Mkuu ahusikae na Mambo ya Nje, Modeste Mutinga, Waziri wa Masuala ya Jamii pamoja na Muhindo Nzangi wa Elimu na vyuo vikuu walisisitiza kumuunga mkono Rais Tshisekedi.

Hii ni mara ya pili Christian Mwando kujiuzulu kutoka serikalini kwa mshikamano na Moses Katumbi. Alifanya vivyo tena mwaka 2015 chini ya utawala wa Joseph Kabila, ambaye Katumbi alimtuhumu kutaka kusalia madarakani.