1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Ethiopia ashinda Nobel

Oumilkheir Hamidou
11 Oktoba 2019

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameshinda Tuzo ya Amani ya Nobel 2019 kutokana na juhudi zake muhimu za kuutatua mzozo wa mpakani na nchi jirani Eritrea.

https://p.dw.com/p/3R7eu
Friedensnobelpreis 2019 Äthiopien | Ministerpräsident Abiy Ahmed
Picha: picture-alliance/dpa/B. Pedersen

Mwenyekiti wa Kamati ya Nobel nchini Norway amesema Berit Reiss-Andersen amesema Abiy mwenye umri wa miaka 43, alichaguliwa kutokana na juhudi zake za kuleta amani na ushirikiano wa kimataifa.

Akielezea sababu za kuchaguliwa waziri mkuu huyo, mwenyekiti wa kamati ya Nobel Bi Berit Reiss-Andersen amesema "Kamati ya Nobel ya Norway imeamua kumtunukia tuzo ya amani ya Nobel, waziri mkuu wa  Ethiopia Abiy Ahmed Ali kwa juhudi zake za kusaka amani na ushirikiano wa kimataifa na hasa kuupatia ufumbuzi mzozo wa mpakani pamoja na nchi jirani ya Eritrea."

Tuzo hiyo imelenga pia kutambua juhudi zote za kuleta amani na masikilizano nchini Ethiopia na katika kanda yote ya Kaskazini Mashariki mwa Afrika.

Ofisi ya waziri mkuu wa Ethiopia imesema katika taarifa yake kwamba tuzo hiyo ni ushindi kwa waethiopia wote na kutoa wito wa kuzidisha hima katika kuifanya Ethiopia iwe upeo wa matumaini mema, na taifa  la neema kwa wote. Taarifa hiyo imemnukuu waziri mkuu huyo mwenye wa miaka 43 akisema wote wana fakhari ya kuwa waethiopia.

Awaangusha vigogo kama Angela Merkel na mwanaharakati kijana wa mazingira, Thunberg.

Waziri mkuu Abiy Ahmed ameingia madarakani tangu April mwaka 2018 kama waziri mkuu, baada ya kujiuzulu Hailemariam Desalegn kufuatia maandamano ya miaka mitatu ya wananchi.

Berlin Kabinett beschließt Klimaschutzpaket
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ni miongoni mwa majina makubwa yaliyojitokeza kwenye orodha ya wagombea wa tuzo hiyo.Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Kabla ya hapo majina kadhaa yalitajwa ikiwa ni pamoja na mwanaharakati wa kupigania usafi wa mazingira, raia wa Sweden, Greta Thunberg mwenye umri wa miaka 16, waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na wanaharakati wanaopigania mageuzi Hong Kong. Idadi ya walioshindania tuzo ya mwaka huu ilijumuisha watu 223 na mashirika 78.

Kama kawaida mshindi atakabidhiwa tuzo hiyo ambayo ni pamoja na kitita cha dola 918.000, medali ya dhahabu na shahada katika sherehe maalumu zitakazofanyika Disemba 10 siku ile ile aliyofariki dunia mwasisi wa tuzo hiyo Alfred Nobel.

Tayari tuzo 99 zimeshatolewa kwa watu na mashirika 24 tangu mwaka 1901. Katika wakati ambapo tuzo zote nyingine zikitangaziwa mjini Stockholm, tuzo hii ya amani hutolewa katika mji mkuu wa Norway, Oslo.

Tayari washindi 11 wa tuzo tufauti za Nobel wameshatangazwa wiki hii, kumi kati yao ni wanaume. Enzi ya uhai wake, Alfred Nobel, mwanaviwanda tajiri wa Sweeden na mgunduzi wa baruti aliusia mshindi wa tuzo hiyo ya amani ya Nobel atunukiwe mjini Oslo.

Sababu halisi ya uamuzi huo haijulikani lakini wakati wa uhai wake Sweeden na Norway zilikuwa zimeungana kabla ya muunganao huo kuvunjika mwaka 1905.