1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu tisa wauwawa Karachi baada ya kifo cha Khamenei

1 Machi 2026

Takriban watu tisa wameripotiwa kufariki na wengine wengi kujeruhiwa katika ghasia na polisi wa kupambana na ghasia mjini Karachi, Pakistan, baada ya waandamanaji kujaribu kuvamia ubalozi mdogo wa Marekani.

https://p.dw.com/p/59cYz
Pakistan Karatschi 2026 |
Waandamanaji waliimba nyimbo za kuilaani Marekani wakielekea eneo la ubalozi wa Marekani.Picha: Akhtar Soomro/REUTERS

Kulingana na msemaji wa hospitali ya Karachi Dkt Jasso Ram, miili tisa imepokelewa na zaidi ya watu 25 wanaendelea kutibiwa, huku idadi ya vifo ikitarajiwa kuongezeka.

Machafuko hayo yamechochewa na taarifa za kifo cha Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei. Waandamanaji waliimba nyimbo za kuilaani Marekani wakielekea eneo la ubalozi, kabla ya maandamano hayo kugeuka na kuwa vurugu, wakijaribu kuvunja kizuizi cha jengo la ubalozi. Polisi walitumia gesi ya machozi na fimbo kusambaratisha umati na kulinda mali za kidiplomasia.

Hata hivyo hali ya usalama imeimarishwa mjini Islamabad, na barabara zote kuelekea eneo la Red Zone mjini humo zimefungwa kwa hofu ya maandamano zaidi.

Huku haya yakijiri makundi ya Palestina ya Hamas na Islamic Jihad, yamepinga mauaji ya Khamenei na kutaja hatua hiyo kama "ujinga wa kivita” na kuzishutumu Marekani na Israel kwa kuhusika moja kwa moja katika yaliyokiita "shambulio la kikatili” lililokiuka uhuru wa Iran na kuathiri usalama wa kikanda.