1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 71 wamekufa kwa kunywa sabuni

Sudi Mnette
22 Desemba 2016

Watu 71 wamekufa kwa kunywa sabuni ya kuogea, wakiifanya kilevi cha gharama nafuu kabisa kwa watu wa kipato cha chini kabisa nchini Urusi.

https://p.dw.com/p/2UiML
Russland Irkutsk Alkoholvergiftungen
Wagonjwa wakipatiwa matibabu katika kliniki ya jiji la Irkustsk nchini UrusiPicha: picture-alliance/dpa/K. Shipitsyn

Watu 71 wamefariki dunia kwa kunywa sabuni ya kuogea yenye sumu katika eneo la Siberia, Urusi, ikiwa mbadala wa kuifanya kama kilevi. Kwa mujibu wa wizara ya afya, jumla ya watu 117 katika jiji la Irkutsk, wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kuzorota kwa afya zao tangu mwishoni mwa juma lililopita na kwamba miongoni mwa hao 71 wameaga dunia. Wanywaji wa kipato duni nchini Urusi wamekuwa na tabia ya kubadili bidhaa nyingine kama manukato na madawa ya kufanyia usafi kuwa kilevi. Vimiminika vya namna hiyo vimekuwa na sumu ambayo inaweza kusababisha kifo hata kama vikitumika kwa kiwango kidogo. Kwa hivi sasa, polisi inawashikilia watu 12 kwa kutengeneza sabuni hizo na kuziuza kwa watu. Kutokana na kadhia hiyo, Rais Vladimir Putin ameiamuru serikali kutumia sheria mpya ifikapo Julai mwakani itakayosimamia uzalishaji na uuzaji wa manukato, mafuta na madawa mengine ya kufanyia usafi yenye ulevi, pamoja na madawa ya mifugo.

Mwandishi: Sudi Mnette AFP

Mhariri: Mohamed Khelef