1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 29 wauwawa Istanbul

Sekione Kitojo
11 Desemba 2016

Mashambulio mawili ya kujitoa muhanga na shambulio la bomu lililotegwa katika  gari karibu na  uwanja  wa  mpira  mjini  Istanbul jana Jumamosi (10.12.2016) yamesababisha  watu 29 kuuwawa na wengine 166 wamejeruhiwa.

https://p.dw.com/p/2U5rV
Türkei Explosion in Istanbul
Magari ya kubebea wagonjwa yakibeba majeruhi mjini IstanbulPicha: Reuters/M. Sezer

Mabomu  hayo  yalilenga maafisa  wa  polisi , na  kuwauwa 27  kati  yao pamoja  na  raia wawili, waziri wa  mambo  ya  ndani  wa  Uturuki, Suleyman Soylu  aliwaambia  waandishi habari  mapema  leo  Jumapili. Ameongeza  kuwa watu 10 wamekamatwa  kwa  kuhusika  na shambulio  hilo  la  kigaidi.

Vifo vya  raia vilikuwa  chini kwasababu  mashabiki walikuwa  wamekwisha  ondoka katika uwanja  huo  mpya  wa  Vodafone Arena  baada  ya  mchezo  wa  mpira  wakati  mripuko  huo wa  bomu  ulipotokea. Watu  walioshuhudia  pia  walisikia  milio  ya  bunduki  baada  ya mripuko.

Türkei Explosion in Istanbul
Moshi ukitoka baada ya shambulio la bomu mjini IstanbulPicha: Reuters/M. Sezer

"Kwa mara  nyingine tumeshuhudia  usiku  wa  leo upande  mwingine  wa  taswira  mbaya  ya ugaidi  ambayo  inakanyaga  kila  maadili  na  utu," rais  wa  Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema  katika  taarifa.

Bomu  la  kwanza  liliripuka  nje  ya  uwanja  maarufu  unaofahamika  kama  Besiktas  baada ya  timu  ya  eneo hilo  kucheza  na  timu  ya  jirani. Mripuko  wa  pili ilikuwa  muda  mfupi baadaye  na  ulielezwa  na  maafisa  kuwa  ni shambulizi  la   kujitoa  muhanga.

Shambulio  la  kigaidi

Polisi  walilifunga  eneo  hilo huku  moshi  ukifuka  kutoka  nyuma  ya  uwanja  huo  na  magari ya  kubebea  wagonjwa  yalianza  kuwapeleka  watu  waliojeruhiwa  hospitali. Vioo  kutoka katika  madirisha  yaliyovunjika  vya  majengo  ya  karibu  vilitapakaa  katika  sehemu  ya wapita  kwa  miguu.

Türkei Explosion in Istanbul
Polisi wakiwasili katika eneo la tukio mjini Istanbul Picha: Reuters/M. Sezer

Hakuna  kundi  ambalo  lilitangaza  kuhusika  na  shambulio  hilo mara  moja. Mwaka  huu, mji wa  Istanbul  umeshuhudia ongezeko  la  mashambulio ambayo  maafisa  wanasema yanafanywa  na  kundi la Dola la Kiislamu ama  kudaiwa  kufanywa  na  wanamgambo  wa Kikurdi.

Hali  ya  hatari  imewekwa  kufuatia  jaribio  lililoshindwa  la  mapinduzi Julai  15.

Soylu alikiri  kwamba  nchi  hiyo  inasumbuka  kuweza  kupambana  na  makundi  kadhaa, yanayojaribu  kukandamiza  mapambano  yake dhidi  ya  ugaidi.

Uturuki  ni  mshirika  katika  muungano  unaoongozwa  na  Marekani  dhidi  ya  kundi  la  Dola la  Kiislamu   na  majeshi  yake  yako katika  nchi  jirani za Syria na Iraq yakipambana na makundi kadhaa ya waasi na Dola la Kiislamu.

Türkei Rede Präsident Recep Tayyip Erdogan in Ankara
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/AP Photo/Presidential Press Service/K. Ozer

Pia  nchi  hiyo  inakabiliana  na  mzozo  mpya  na  kundi  lililopigwa  marufuku  la  Wakurdi upande  wa  kusini  mashariki  mwa  nchi  hiyo.

Ned Price , msemaji  wa  baraza  la  usalama  wa  taifa  nchini  Marekani , amesema Marekani  inalaani  shambulio  hilo , kwa  kiwango  cha  juu  kabisa.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape

Mhariri: Yusra Buwayhid