1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUganda

Watu 11 wauawa katika mashambulizi mawili ya waasi Beni

Bruce Amani
25 Machi 2024

Karibu watu 11 wameuawa katika mashambulizi mawili yaliyofanyika karibu na mji wa Beni, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4e4v1
Wanajeshi wa Kongo wakishika doria Beni
Uganda ilianzisha operesheni ya pamoja na jeshi la Kongo kuwasaka waasi wa ADFPicha: Alain Uaykani/Xinhua News Agency/picture alliance

Hayo ni kwa mujibu wa maafisa wa eneo hilo waliosema mashambulizi hayo yalifanywa na kundi la waasi wa ADF. Augustin Kapupa, afisa katika eneo la Matembo ambako shambulizi la kwanza lilifanyika, amesema raia sita waliuawa katika tukio hilo la Jumamosi usiku.

Mzee wa mtaa Antoine Kambale amesema baada ya mauaji yaliyofanywa na ADF katika eneo la Matembo, waasi hao walivamia kijiji cha Sayo na kuwauwa watu watano. Afisa wa mji wa Beni Makofi Bukuku ameliambia shirika la habari la AFP kuwa idadi ya vifo katika eneo la Sayo huenda ikaongezeka, kwa sababu waasi bado wako katika eneo hilo.

Soma pia: Mapigano makali yazuka upya mashariki mwa Kongo

Kiongozi wa mashirika ya kijamii katika eneo la Matembo Germain Kathemika amesema wakaazi walikuwa wakilionya jeshi kuhusu hatari inayosababishwa na uwepo wa waasi katika eneo hilo kwa wiki tatu zilizopita. Jeshi la Kongo halijazungumzia mashambulizi hayo.