Mapigano makali yazuka upya mashariki mwa Kongo
18 Machi 2024Duru za kijeshi na za asasi za kiraia Jimboni Kivu ya Kaskazini zimeripoti mapigano makali kwenye mji wa Sake na vitongoji vyake. John Banyene, kiongozi wa asasi za kiraia kwenye jimbo la Kivu ya Kaskazini amesema milio ya risasi na mizinga vimesikika kuanzia saa 11 Aflajiri kwenye mji wa Sake umbali wa kilomita 27 na mji wa Goma.
''Toka asubuhi kumekuwa na mapigano, hata mabomu kutoka upande wa waasi yamekuwa yakianguka karibu na makambi ya wakimbizi huko Mugunga. Huko Kasengesi pia mabomu mawili yameanguka. Hali hii inaendelea kuzusha wasiwasi kwa raia na wakimbizi.'', alisema Banyene.
Mapigano yalizuka upya Jumamosi baada ya siku kadhaa ya utuluvu kwenye eneo hilo. Waasi wa M23 wamekuwa wakijaribu kuuteka mji wa Sake ambao ni ngome muhimu ya jeshi la Kongo. Umoja wa Mataifa umesema wanajeshi wake wanane walijeruhiwa kwa bomu. Bintou Keita, mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo, Monusco, amelaani shambulizi hilo. Na kutoa mwito kwa waasi wa M23 kuweka chini silaha.
Kwenye taarifa yake hapo jana, kundi la waasi wa M23 liliwatuhumu wanajeshi wa Monusco kwa kushirikiana na jeshi la Kongo na wanamgambo wa FDLR na makundi mengine ya wapiganaji. Kwa siku kadhaa sasa barabara muhimu zinazoelekea mji wa Goma zimedhibitiwa na waasi wa M23. Hali ambayo imezusha wasiwasi mkubwa kwa raia wa mji huo wenye wakaazi miloni moja.
Maelfu ya raia wa Kivu ya Kaskazini waendelea kukimbia
John Banyenye, kiongozi wa asasi za kiaraia huko Kivu ya Kaskazini ametoa wito kwa serikali ya Kongo kutafuta suluhisho la haraka.
''Wakimbizi wanaishi kwa tabu sana kwa kukosa chakula na huduma zingine. Ndio sababu tunaitaka serikali ya Kongo na wadau wake kushughulikia haraka mzozo huu wa Kivu ili wakimbizi warejee makwao.''
Akihitimisha zaiara yake mwishoni mwa wiki huko mjini Goma, mwakilishi wa ofisi ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masaula ya dharura, OCHA, Ramesh Rajasingham alielezea wasiwasi wake kuhusu kuzingirwa kwa mji wa Goma na makundi yenye silaha huku akielezea hali ya wakimbizi wa ndani kuwa ni mbaya zaidi.