1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiga kura kuamua hatima ya Komoro

11 Mei 2016

Wapiga kura wa Komoro wanatoa sauti zao katika zoezi la uchaguzi katika vituo 13 kisiwani Nzuwani. Zoezi hilo litaamua nani kati ya mgombea wa upinzani Azali Assoumani na wa chama tawala Mamadou atashinda.

https://p.dw.com/p/1IlXf
Wafuasi wa Kongamano la wapenda demokrasia Komoro katika kampeni yao february 23 mwaka 2015 katika mji mkuu MoroniPicha: Getty Images/AFP/M. Longari

Mamia ya wapiga kura wamekuwa wakisubiri kwa utulivu leo asubuhi mbele ya shule ya Mramani-kijiji cha kusini mwa kisiwa cha Nzuwani.

Wanajeshi zaidi ya mia moja, wakiwemo pia wale wa usalama,bunduki mkononi,wanailinda shule hiyo vinakokutikana vituo 13 ambako zoezi hilo la aina pekee la uchaguzi linaendelea. Zoezi hilo linafanyika kwa kuwa wapiga kura wa eneo hilo walishindwa kutekeleza jukumu lao kufuatia machafuko yaliyoripuka duru ya pili ya uchaguzi wa rais na magavana ulipopitishwa visiwani Comoros, April 10 iliyopita.

"Hatukuweza kupiga kura mara ya mwisho,lakini leo,wanajeshi wanatulinda,mie na mume wangu ambae haoni" amesema Bweni Aboudou aliyekuwa miongoni mwa wa mwanzo kupiga kura vituo vilipofunguliwa saa moja asubuhi.

Duru ya pili ya uchaguzi katika visiwa hivyo vidogo vya bahari ya Hindi iligubikwa na machafuko hasa katika kisiwa cha Nzuwani ambako vituo vya kupiga kura vilivunjwa na watu kusumbuliwa.

Hatua za usalama zimeimarishwa ili kuepusha udanganyifu

Jumla ya wapiga kura 6305 waliosajiliwa katika vituo 13 vya Mramani walishindwa kutekeleza wajibu wao Aprili 10 iliyopita-hayo ni kwa mujibu wa korti ya katiba iliyoamuru zoezi la uchaguzi lirudiwe katika eneo hilo.

Karte Komoren Mayotte englisch
Ramani ya visiwa vya Komoro katika bahari ya HindiPicha: DW

Tangu asubuhi wanajeshi wamezifunga njia ziote zinazoelekea katika shule ya Mramani vinakokutikana vituo vyote 13 vya kupiga kura. Watu wenye vibali maalum tu ndio wanaoruhusiwa kupita na magari-hatua hiyo imechukuliwa ili miongoni mwa mengineyo kuzuwia mbinu za udangayifu wakati wa uchaguzi.

"Kwa sasa mambo yanaendelea vizuri. Hatua zote zinazohitajika zimechukuliwa ili kuepusha vurugu-amesema hayo Mariana Massoundi ambaye ni afisa wa tume ya uchaguzi-CENI.

Mgombea wa upande wa upinzani Azali Assoumani ameonyesha kuridhika akisema "ikiwa usalama utaimarishwa hakutakuwa na sababu ya yeye kutochaguliwa kuwa rais Mungu akipenda-amesema huku akitabasamu kanali huyo wa zamani wa jeshi. Anajivunia uungaji mkono wa rais wa zamani wa Komoro Ahmed Abdallah Sambi anaetokea katika kisiwa hicho hicho cha Nzuwani na ambako ni mashuhuri kupita kiasi.

Raisi mteule ataapishwa rasmi May 26

Kwa upande wake Mohammed Ali Swalihi,maarufu kwa jina "Mamadou" anasema "amepania kweli kweli na ana matumaini kuliko zamani. Mamadou anaungwa mkono na mgombea mwenzake katika duru ya pili ya uchaguzi,gavana wa kisiwa cha Ngazija Mouigni Baraka Said Soilihi.

Ahmed Abdallah Mohamed Sambi Präsident Komoren
Rais wa Zamani wa Komoro Ahmed Abdallah Mohammed SambiPicha: picture-alliance/ dpa

Vituo vya kupiga kura vitafungwa saa 12 kwa saa za Afrika mashariki na matokeo yanaweza kutangazwa leo usiku au pengine Alkhamisi-wakati rais mpya anatarajiwa kuapishwa kama ilivyopangwa May 26 inayokuja.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Gakuba Daniel