Wanawake wenye nguvu zaidi Afrika
Wanawake barani Afrika wanapambana na jamii inayoongozwa kisiasa na kiuchumi na wanaume na licha ya changamoto iliopo baadhi ya wanawake wanaonekana kuongoza. Hawa ni wanawake tisa wenye nguvu zaidi barani Afrika.
Rais wa kwanza mwanamke Afrika
Ellen Johnson Sirleaf alikuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa rais barani Afrika. Kama rais wa Liberia kutoka mwaka 2006 hadi 2018, alipambana na ukosefu wa ajira, deni la taifa, na ugonjwa wa Ebola. Johnson Sirleaf alishinda tuzo ya amani ya Nobeli mwaka 2011 kufuatia jukumu lake la kuimarisha usalama na haki za wanawake.
Hatua kubwa kwa wanawake Ethiopia
Sahle-Work Zewde ndio rais wa Ethiopia, tangu Oktoba 2018. Wadhifa huo ni wa heshima kutokana na kwamba maamuzi yote anayo waziri mkuu na baraza la mawaziri. Uchaguzi wa Zewde unaangaliwa kama hatua kubwa kwenda mbele nchini Ethiopia ambako wanaume wanaongoza katika siasa na biashara. Nusu ya wajumbe wa baraza la mawaziri nchini humo ni wanawake.
Katibu Mkuu wa Francophonie 2019
Louise Mushikiwabo, aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Rwanda, ndiye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya mataifa yanayozungumza kifaransa Francophonie 2019. Mushikiwabo alichaguliwa licha ya kwamba Rwanda imekifanya Kingereza kuwa lugha inayotumiwa kiutawala, biashara na elimu badala ya kifaransa kama ilivyokuwa awali. Uteuzi wake unaonekana kama ushindi wa kidiplomasia ulioungwa mkono na Ufaransa.
Mwanamke mmoja na majimbo 193
Amina Mohammed raia wa Nigeria amekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa tangu Januari 2017. Alifanya kazi na shirika hilo la UN juu ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia kuanzia 2002 hadi 2005, baadaye akafanya kazi kama mshauri maalum wa katibu mkuu wa wakati huo Ban Ki Moon na kuhudumu mwaka mmoja kama waziri wa mazingira nchini Nigeria chini ya utawala wa rais Muhammadu Buhari.
Mpiganaji dhidi ya madeni usukani mwa serikali
Nchini Namibia, Waziri Mkuu Saara Kuugongelwa-Amadhila ameiongoza serikali kuanzia Machi mwaka 2015, alipokuwa mwanamke wa kwanza kupata nafasi hiyo. Aliwahi kufanya kazi kama waziri wa fedha akiwa na malengo ya kupunguza madeni ya taifa hilo. Mwanauchumi huyo amekuwa mjumbe wa bunge la Namibia tangu mwaka 1995.
Bintimfalme wa mafuta aliepoteza sifa
Isabel dos Santos, mtoto wa rais wa zamani wa Angola Jose dos Santos, ni moja ya matajiri wakubwa wa kike Afrika. Alipata baadhi ya utajiri wake baada ya babaake kumpa cheo cha ukurugenzi katika kampuni ya taifa ya mafuta mwaka 2016. Rais mpya wa Angola alimuondoa katika nafasi hiyo na kuanzisha uchunguzi wa ufisadi katika sekta ya mafuta.
Mwanamke mwenye ushawishi DRC
Jaynet Kabila, pacha wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Joseph Kabila na mtoto wa rais wa zamani wa taifa hilo Laurent Kabila, anajulikana kwa usiri wake na udhalimu. Ni mbunge anaemiliki kituo cha televisheni, kampuni ya mitandao na radio. Mwaka 2015, jarida la Ufaransa la Jeune Afrique lilimtangaza kuwa moja ya watu walio na ushawishi serikalini.
Waziri aliyeweka historia
Kamissa Camara, mwanamke wa kwanza kijana kuwa waziri wa mambo ya kigeni katika historia ya Mali ni mpya kabisa katika sera za kigeni. Waziri huyo mwenye umri wa miaka 35 aliteuliwa kuingia bungeni na rais Ibrahim Boubacar Keita na sasa ni mmoja wa wanawake 11 katika baraza la mawaziri lililo na mawaziri 32 nchini Mali.
Mafanyabiashara tajiri wa mafuta Nigeria
Utajiri wa Folorunsho Alakija raia wa Nigeria unatajwa kufika dola bilioni 1.6. Uzalishaji wa mafuta nchini Nigeria unamfanya bibi huyo mmiliki wa kampuni ya mafuta ya Famfa Oil kuwa mtu wa tatu kwa utajiri nchini humo. Jarida la Forbes limemuorodhesha kuwa miongoni mwa watu matajiri duniani. Folorunsho Alakija mwenye umri wa miaka 67- ana taasisi inayowasaidia wajane na mayatima.