1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Wanajeshi 7 wa Israel wauwawa kwenye mapigano Ukanda wa Gaza

13 Desemba 2023

Wanajeshi wasiopungua saba wa Israel wameuawa kwenye shambulizi katika mji wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4a6Jz
Ukanda wa Gaza baada ya mashambulizi ya Israel
Moshi ukifuka Ukanda wa Gaza baada ya mashambulizi ya Israel.Picha: MAHMUD HAMS/AFP/Getty Images

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti hayo leo, wakati jeshi la nchi hiyo likikabiliwa na upinzani mkali katika vita vyake dhidi ya Hamas.

Aidha, mashambulizi ya Israel yamezusha ghadhabu ya kimataifa na ukosoaji wa nadra kutoka Marekani kuhusu mauaji ya maelfu ya raia.

Utawala wa rais Joe Biden umekuwa ukitoa wito wa mara kwa mara kwa Israel kuchukua hatua kubwa zaidi kuwaepusha raia wa Palestina dhidi ya maafa.

Katika tukio jingine hapo jana, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio linalotaka usitishaji mapigano mara moja katika Ukanda wa Gaza kwa sababu za kibinadamu.

Nchi 153 zililiunga mkono azimio hilo na 10 zililipinga. Ujerumani ni miongoni mwa nchi 23 ambazo zilijizuia kupiga kura kwa madai ya azimio hilo kuwa la jumla jamala na kutotaja haki ya Israel kujilinda.