1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya wanaoacha shule yaongezeka Ujerumani

Lilian Mtono
20 Februari 2024

Ikilinganishwa na nchi nyingine za Ulaya, Ujerumani ina idadi kubwa ya vijana wasio na diploma ya shule au sifa zozote za ufundi stadi. Sasa tatizo ni kubwa sana

https://p.dw.com/p/4caHr
Picha ya shule ya chekechea, Ujerumani
Wanafunzi wakiwa darasani katika shule ya chekechea. Ujerumani inakabiliwa na ongezeko la wanafunzi wanaoacha shule kabla ya kupata stashahadaPicha: Sebastian Gollnow/dpa/picture alliance

Mtu yeyote anayetafuta kazi nchini Ujerumani anapaswa kuipata mara moja: Zaidi ya nafasi za kazi milioni 1.7 zilirekodiwa katika majira ya joto ya mwaka 2023. Mahitaji ya wafanyakazi wenye ujuzi katika taaluma zipatazo 200 yanazidi idadi ya waombaji, na kuna hitaji kubwa la watumishi kwenye sekta ya tiba na uuguzi, wafanyakazi wa ujenzi, teknolojia ya mawasiliano, madereva wasomi, walimu na wengine wengi.

Lakini kimahesabu, uhaba huu haupaswi kuwepo. Mwanzoni mwa mwaka 2024, karibu watu milioni 4.8 ambao wanaweza kufanya kazi walipata marupurupu ya kukosa na ajira.

Hata hivyo, zaidi ya nusu ya hao hawajamaliza mafunzo ya ufundi stadi. Kulingana na Shirikisho la Ajira, fursa yao ya kupata kazi ni ndogo. Takwimu nyingine ya kushangaza ni asilimia 25 ya watu wasio na ajira kwa muda mrefu ambao hawana stashahada ya shule ya aina yoyote.

Ujerumani iko nyuma sana

Kwa miaka mingi, mashirika ya kimataifa kama vile Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) yamekuwa yakikosoa hatua ndogo zinazochukuliwa na Ujerumani katika kupunguza idadi ya watu wasio na sifa zozote.

Waziri wa elimu wa Ujerumani Stark-Watzinger
Waziri wa Elimu na utafiti wa serikali ya shirikisho la Ujerumani Bettina Stark WatzingerPicha: IMAGO/Achille Abboud

Mfumo wa elimu wa Ujerumani umeweza kupata vijana wengi kupitia shule za upili na vyuo vikuu kuliko hapo awali. Hata hivyo, bado kuna idadi kubwa ya watu ambao hawawezi kukidhi mahitaji ya chini zaidi yaliyowekwa na waajiri wakubwa.

Kila mwaka, Ofisi ya Takwimu ya Ulaya (Eurostat) hukusanya takwimu za vijana wa kati ya umri wa miaka 18 na 24 katika nchi za Ulaya ambao hawamalizi shule au mafunzo ya ufundi stadi. Mnamo 2022, kiwango kilikuwa 12%. Kati ya nchi 27 za Umoja wa Ulaya, Ujerumani ilishika nafasi ya nne kutoka mwisho.

Soma pia:Zaidi ya Wajerumani milioni 4 walitafuta ajira mwaka 2019.

Takwimu za kuacha shule pia zinajumuisha vijana wanaomaliza kiwango cha msingi zaidi cha elimu ya lazima nchini Ujerumani, ambayo humalizika baada ya mwaka wa 10 wa masomo.

Nchini Ujerumani, watoto husoma pamoja kwa miaka minne hadi sita kabla ya kupangiwa shule tofauti za sekondari kulingana na uwezo wao wa kitaaluma. Elimu ni jukumu la majimbo 16 ya shirikisho na kwa hivyo mifumo ya shule inatofautiana kutoka jimbo hadi jimbo. Kuna wanafunzi walioacha shule katika kila jimbo, na mwaka 2022 pekee karibu wanafunzi 52,000 waliacha.

Idadi kubwa ya wanafunzi wa mataifa ya kigeni miongoni mwa wanaoacha shule

Sababu hasa ya kuwa na wasiwasi ni kutokana na ukweli kwamba wengi wanaoacha shule ni vijana wenye asili ya uhamiaji, kulingana na utafiti wa Taasisi ya Shirikisho ya Utafiti wa Idadi ya Watu (BiB).

Ujerumani, Berlin | Wakimbizi wa Ukraine
Mwalimu Tatjana akiwafundisha wanafunzi wa chekechea mjini Berlin, Ujerumani. Watoto hawa walikimbia vita nchini Ukraine Picha: Maja Hitij/Getty Images

Mnamo 2022, hata hivyo asilimia 3% tu ya wanaume wa Ujerumani wenye umri wa miaka 25 na 2% ya wanawake wasio na asili ya uhamiaji hawakuwa na stashahada ama diploma.

Soma pia:Merkel na mawaziri wake wazungumzia ustawi

Wataalamu wa elimu kwa muda mrefu wamekosoa mfumo wa shule wa Ujerumani unaowaacha vijana wengi kando. Katika jaribio la hivi karibuni zaidi la Pisa, linalinganisha ujuzi wa kusoma, hesabu na sayansi wa watoto wa miaka 15 kimataifa na wanafunzi wa Ujerumani walipata alama za chini zaidi kuwahi kurekodiwa .

Ujuzi mdogo wa lugha ya Kijerumani

Matatizo yanaanzia chekechea. Mtoto mmoja kati ya watano wenye umri wa kati ya miaka mitatu na sita sasa hazungumzi Kijerumani akiwa nyumbani. Katika majimbo ya Hesse, Berlin na Bremen, idadi hiyo ni ya juu sawa na theluthi.

Na hii inafanya kuwa na umuhimu zaidi kwa watoto hawa kwenda shule za chekechea. Hata hivyo, kulingana na ripoti ya elimu ya serikali ya Ujerumani, ni 81% tu ya watoto wenye asili ya uhamiaji hufanya hivyo.

Wanafunzi waliohitimu mafunzo ya chuo Kikuu
Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Bonn nchini Ujerumani wakiwa kwenye mahafali Julai 14, 2012. Picha: Rainer Unkel/Imago Images

Hiyo ni kwa sababu kuna uhaba wa maeneo ya kulelea watoto, ambayo kwa sasa ni yanakaribia 350,000 kote Ujerumani. Ikiwa watoto hawazungumzi Kijerumani wanapoanza shule, wanaweza kurudi nyuma kimasomo. Hii inaweza kuwashusha daraja.

Upungufu mkubwa wa wataalamu mashuleni

Kwa sasa kuna uhaba wa walimu 14,000 wa ziada nchini Ujerumani na idadi hiyo inaonekana kuongezeka.

Anja Bensinger-Stolze, ambaye ni mjumbe wa bodi ya Chama cha Wafanyakazi wa Elimu na Sayansi, ameiambia DW kwamba "Kwa bahati mbaya, wanasiasa wameichukulia hali hiyo kirahisi sana kwa muda mrefu. Kwa hiyo, ni vigumu sana kupunguza au kuboresha hali hiyo kwa muda mfupi."

Hiyo ni habari mbaya kwa wanafunzi wanaohitaji msaada mkubwa. Baada ya yote, programu zinazolenga kupunguza idadi ya wanaomaliza shule za mapema pia ziko hatarini. Katika baadhi ya majimbo ya shirikisho, kwa mfano, kuna mradi wa "Productive Learning" unaowalenga kuwapata vijana walio katika hatari ya kufeli baada ya darasa la nane kwa kuwapa fursa ya kufanya lile wanaloliweza zaidi ili hatimaye kupata kazi zinazowafaa.

Mkuu wa wakala wa ajira, Andrea Nahles sasa amependekeza kuanza mwongozo wa kazi mashuleni kuanzia madarasa ya chini kama darasa la tano.