1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa kupambana na mihadarati Afrika wakutana Tanzania

Hawa Bihoga17 Septemba 2018

Biashara ya mihadarati hufadhili kwa kiwango kikubwa masuala ya ugaidi huku matokeo yake ya fedha zilizotajwa kuwa ni haramu zikiongeza ustawi wa vitendo vya rushwa katika mataifa ya  Afrika.

https://p.dw.com/p/352BF
Tansania Repräsentanten im Kampf gegen Drogenmißbrauch
Picha: DW/H. Amri

Inaarifiwa kuwa biashara ya dawa za kulevya aina ya heroin na cocaine hufadhili kwa kiwango kikubwa masuala ya ugaidi huku matokeo yake ya fedha ziliozotajwa kuwa ni haramu zikiongeza ustawi wa vitendo vya rushwa katika mataifa ya  Afrika. Hayo yamebainika katika mkutano wa ishirini na nane unaowakutanisha wakuu wa vyombo vinavyopambana na dawa za kulevya barani Afrika ambapo nchi zaidi ya Hamsini zinashiriki mjini Dar es Salaam.

Mkutano unaanza kwa kubainishwa kwa ukubwa wa tatizo Afrika, ambapo inaelezwa kwamba takriban tani mia mbili za dawa za kulevya zinapitishwa katika ukanda wa Afrika ya mamshariki, ikitokea ukanda wa Sahel na pembe ya Afrika na kuelekea katika mabara mengine.

Usafirishaji huo unatajwa kuwa katika mfumo madhubuti na ulioshirikishi  kwa kiwango kikubwa, unanyooshewa kidole na nchi hizo kuwa ni wafadhili wakubwa katika masuala ya ugaidi ambayo yamekuwa yakishuhudiwa katika baadhi ya nchi na kughalimu maisha ya watu.

Watumiaji wa mihadarati waongezeka Afrika: Utafiti

Inaelezwa kwamba takriban tani mia mbili za dawa za kulevya zinapitishwa katika ukanda wa Afrika ya mamshariki, ikitokea ukanda wa Sahel na pembe ya Afrika na kuelekea katika mabara mengine.
Inaelezwa kwamba takriban tani mia mbili za dawa za kulevya zinapitishwa katika ukanda wa Afrika ya mamshariki, ikitokea ukanda wa Sahel na pembe ya Afrika na kuelekea katika mabara mengine.Picha: Fotolia/Africa Studio

Hili linaiweka bara la Afrika katika ramani ya dunia kuwa ni miongoni mwa njia kuu ya kupitishia dawa za kulevya, ijapokuwa utafiti unaonesha kwamba watumiaji wanaongezeka katika bara hilo, hivyo na lenyewe kuwa ni sehemu ya soko la uhakika la dawa hizo haramu.

Mwakilishi wa shirika la umoja wa mataifa linalopambana na dawa za kulevya na uhalifu UNODC, kwa ukanda wa Afrika mashariki  dokta  Amado Andres, ameuwambia mikutano huo kuwa, changamoto ya dawa za kulevya inaathari  jamii kiusalama, kiafya na hata kiuchumi. 

Hata hivyo mikutano unabainisha kuwa, licha ya udhibiti mkubwa wa dawa za kulevya katika mataifa hayo 54 yalioshiriki, mbinu nyingine ya matumizi ya dawa za binadamu kama dawa za kupunguza maumivu na za kuleta usingizi zinapotoshwa matumizi na kuwa kama dawa za kulevya, hii ni kutokana na urahisi wa upatikanaji wake, na hivyo mkutano kutaka hili pia kuwa ni miongoni mwa ajenda muhimu za kujadiliwa ndani ya mkutano huo.

Katika hili nchi ya Tanzania  kupitia waziri mkuu wake Kasim Majaliwa, amesema anaona ni vyema kuwa na sheria madhubuti ambayo itafanya kazi katika mataifa yote ya Afrika ili kuififisha biashara hiyo inayotajwa kuwa na mtandao mpana na madhubuti ulimwenguni.

Mkutano huu wa siku tano wenye washiriki zaidi ya mia moja kutoka mataifa 54 ikiwemo Kenya,Uganda, Sudan, Nigeria, Mali  na mwenyeji Tanzania unatarajiwa kuja na hoja za kufanyia kazi kwa nchi washiriki.

Mwandishi: Hawa Bihoga Dw Dar es Salaam

Mhariri: Mohammed Khelef