1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Wakazi wa Uingereza wajutia uamuzi wa Brexit

Lilian Mtono
2 Februari 2023

Ikiwa ni miaka mitatu sasa tangu Uingereza ilipojiondoa kikamilifu kwenye Umoja wa Ulaya, baadhi ya wakazi nchini humo wanaeleza kujutia uamuzi huo wakiiona Uingereza kama meli isiyo na nahodha.

https://p.dw.com/p/4N0N9
Großbritanniens Premierminister Boris Johnson
Picha: Frank Augstein/AP Photo/picture alliance

Ni mwaka wa tatu sasa tangu Uingereza ilipojiondoa kabisa kwenye Umoja wa Ulaya ama Brexit. Miaka ikizidi kusonga mbele maoni yameanza kutofautiana wakati baadhi ya waliokuwa wakipigania kujitenga na Umoja huo sasa wakitamani kurejea lakini wengine wakisalia na misimamo ileile. Hali mbaya ya kiuchumi na kimaisha nchini humo inawafanya wengi kuona ya kwamba hakukua na sababu ya kujiondoa.

Grays, ni mji ulioko karibu na jiji la London ambako wakazi wake walipiga kura kwa wingi kuunga mkono Brexit. Lakini miaka mitatu baadaye baada ya mahusiano ya London na Umoja wa Ulaya kuwa mabaya, baadhi wanatamani kuibadilisha ile kura waliyopiga hapo kabla na hasa kutokana na taifa hilo kujikuta likiingia kwenye mizozo ya kila wakati.

Maria Yvars mwenye miaka 42 anakiri kwamba alipiga kura kutaka Brexit  lakini sasa anajuta kwa sababu anasema wanasiasa waliwadanganya. Anasema hawakuwaambia ukweli wa kina kuhusu Brexit.. akaongeza kila walichowaambia hakikuwa na ukweli wowote. Maria anaiona Uingereza kama meli bila ya kapteni akizingatia mtikisiko wa hivi karibuni wa kisiasa ndanoi ya chama cha Conservative, uliosababisha mawawziri wakuu kujiuzulu, ikiwa ni pamoja na Boris Johnson aliyeongoza kampeni ya Brexit.

Brexit-Folgen in UK | London steigende Inflation und leere Lebensmittelregale der Supermärkte
Wengi wa raia nchini Uingereza wanalia kutokana na hali mbaya ya kiuchumi na mfumuko wa bei. Picha: JUSTIN TALLIS/AFP

Soma Zaidi: Uingereza yatetea uamuzi wake wa kujiondoa kutoka kwenye Umoja wa Ulaya licha ya kubanwa na matatizo ya kiuchumi

Kwenye kura ya kujiondoa ya mwaka 2016, asilimia 72.3 walipiga kura ya kujitenga na Umoja wa Ulaya katika jimbo la Essex, uliko mji wa Grays na ambao una wakazi wengi wapatao 75,000. Mji huu ulishika nafasi ya nne kati ya maeneo yaliyokuwa na idadi kubwa ya kura za kuunga mkono hoja hiyo nchini Uingereza.

Shirika la habari la AFP lililoripoti mchakato mzima wa upigaji kura kwenye eneo hilo, liliwakuta wakazi wakiendelea na masiah kama kawaida mwaka mmoja baada ya Brexit. Lakini wakati huo bado Uingereza ilikuwa haijakamilisha mchakato wa kujitenga na Umoja huo, ambao hatimayde ulikamilika Januari 2020.

Soma Zaidi: Ulaya yawasilisha mapendekezo kuepusha mzozo mpya wa Brexit

Yale yaliyoahidiwa na wanasiasa hayajatekelezeka hadi sasa.

Johnson aliahidi Uingereza itakuwa nchi ya maziwa na asali, lakini badala yake, ikakumbwa na janga la UVIKO-19 na sasa hali ngumu ya maisha iliyoachangiwa na kupanda kwa gharama na mfumuko mkubwa kabisa wa bei. Na mamlaka ya halmashauri ya Thurrock kunakopatikana mji huu wa Grays, zilifilisika kwa muda mwezi Disemba kufuatia uwekezaji ambao haukuwa na maslahi. Maduka yakafungwa kama ilivyo katika miji mingine yenye shughuli nyingi nchini Uingereza. Na sasa majengo ya maduka hayo ndiko unaweza kukuta bidhaa zinazouwa kwa bei ya chini ya hadi pauni 1, ama maeneo ya kutoa misaada kwa wasiojiweza.

Ingawa serikali inajaribu kuwaeleza watu wake ya kwamba kinachotokea sasa kimechochewa na janga la corona na vita vya Ukraine, lakini Brexit ina mchango mkubwa kwa kuwa imekata mianya iliyounganisha taifa hilo na soko la pamoja la Ulaya kupitia ujia unaotokea Essex.

Soma Zaidi: Uhaba wa mafuta Uingereza waathiri huduma muhimu kama uuguzi

Großbritannien London | Rishi Sunak
Waziri mkuu wa uingereza Rishi Sunak bado hajafanikiwa kutoa ushsawishi wa kutosha wa namna ya kukabiliana na hali ya mambo.Picha: Tayfun Salci/ZUMA Press/picture alliance

Mwanamke mmoja wa miaka 50 anakiri kwamba alipiga kura ya kujiondoa, lakini sasa anajutia uamuzi wake. Anasema anachoona sasa ni janga tu na kuongeza kuwa wengi anaowafahamu wanajutia uamuzi wao wa kutaka kujitenga na Umoja wa Ulaya.

Lakini si waziri mkuu Rishi Sunak wa chama cha Conservative ama Labour kwa upande wa upinzani wanaotoa ahadi ya mabadiliko ya hali ilivyo na badala yake wakiwahakikishia wananchi kuendelea kuamini kuhusu Brexit.

Ni Waingereza wachache mno, chini ya theluthi moja wanaoendelea kuamini kwamba uamuzi wa Brexit ulikuwa ni mzuri, huku mmoja kati ya watano waliotaka kujitoa akionekana kubadilisha mtizamo wake, hii ikiwa ni kulingana na ripoti ya uchunguzi uliofanywa na taasisi ya YouGov iliyochapishwa Novemba mwaka uliopita.

Lakini Elaine Read, mama wa umri wa miaka 73 wala hajutii uamuzi wake wa kutaka kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya. Anasema hata kura ingepigwa tena hii leo, asingejali kuunga tena mkono uamuzi huo. Anajigamba kwamba ni kama wako kisiwani, waliojitenga. Anasema hapo kabla aliona kama hawakuwa na udhibiti wa mambo yao na sheria nyingi zilibadilishwa na Brussels, makao makuu ya Umoja wa Ulaya. Anasema mengi yanajitokeza kwa sasa ambayo hayakuwahi kutokea huko nyuma na sasa wanaona faida yake.