1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkwamo wa Brexit waendelea kati ya EU na Uingereza

Mohammed Khelef
7 Desemba 2020

Mkuu wa timu ya upatanishi ya Umoja wa Ulaya kwenye mazungumzo ya BREXIT, Michael Barnier, asema hakuna maendeleo ya maana yaliyofikiwa licha ya shinikizo kubwa kuelekea muda wa mwisho uliowekwa kukaribia.

https://p.dw.com/p/3mKgY
UK Michel Barnier
Picha: Peter Nicholls/REUTERS

Hayo yanakuja huku Uingereza yenyewe ikikataa kuongezwa muda kwa kipindi cha mpito baada ya mwisho wa mwaka huu. 

Mkwamo kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya hadi sasa upo kwenye masuala matatu muhimu, ambayo ni kujenga mazingira ya usawa kwenye ushindani wa kibiashara, kusaka makubaliano ya masuala ya uvuvi na pia mambo yanayohusiana na usimamizi na uendeshaji wa mambo hayo, na kwa mujibu wa Barnier, hakuna chochote kilichoafikiwa baina yao kwenye masuala hayo.

Baada ya yeye na mwenzake anayewakilisha Uingereza kwenye mazungumzo hayo, David Frost, kuomba muda wa mapumziko siku ya Ijumaa kutokana na kukwama kwenye majadiliano yao, Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen, na Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, waliwaagiza kuendelea na mazungumzo yao mjini Brussels.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson (kushoto) na Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen (kulia)
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson (kushoto) na Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen (kulia)Picha: Peter Summers/Getty Images

Majadiliano ya Brexit hatihati kuvunjika

Jioni hii, wabunge nchini Uingereza watajadili na kuupigia kura mswaada wenye utata juu ya Masoko ya Ndani, ambao unaanzisha sheria ya kuratibu biashara miongoni mwa mataifa manne yanayounda Ufalme wa Uingereza, baada ya kujitowa kwenye Umoja wa Ulaya.

Awali mswaada huo ulifanyiwa marekebisho na Baraza la Mamwinyi kwenye bunge la Uingereza, kuondoa kipengele ambacho kilikuwa kimewakasirisha maafisa wa Umoja wa Ulaya. Kipengele hicho, ambacho kinawapa wabunge madaraka ya kuunda kanuni juu ya msaada wa serikali na taratibu za forodha kwa bidhaa zinazotoka Ireland ya Kaskazini kwenda Uingereza, kingelikuwa kinavunja Kifungu Nambari 4 cha sheria ya Uingereza inayosimamia kujiondowa kwake kwenye Umoja wa Ulaya.

 

Mpango wa Uingereza waibua wasiwasi Umoja wa Ulaya

Ripoti za vyombo vya habari zinasema kwamba jana jioni ilikuwa karibuni kufikiwa kwa makubaliano juu ya masuala ya uvuvi, lakini kisha Ufaransa ikatishia kwamba ingelipigia kura ya turufu dhidi ya makubaliano yoyote ambayo yasingeheshimu haki na maslahi ya wavuvi wake.

Mkuu wa timu ya mashauriano wa Umoja wa Ulaya Michel Barnier na mshauri wa waziri mkuu wa Uingereza kuhusu Ulaya David Frost.
Mkuu wa timu ya mashauriano wa Umoja wa Ulaya Michel Barnier na mshauri wa waziri mkuu wa Uingereza kuhusu Ulaya David Frost.Picha: Oliver Hoslet/REUTERS

Wakosoaji wameonya kwamba hatua ya wabunge wa Uingereza kupitisha sheria inayovunja makubaliano ya kimataifa kati ya nchi hiyo na Umoja wa Ulaya kutaondosha imani ya Umoja huo na washirika wengine. Hata hivyo, Uingereza inashikilia kwamba hatua kama hiyo ni kwa ajili ya kuyalinda masoko yake ya ndani.

Waziri wa Masuala ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini kwenye serikali ya Johnson, James Cleverly, alikiambia kituo cha Sky News mapema leo kwamba kipengele hicho kitaongezwa tena kabla ya kura ya leo, ikimaanisha kwamba kinaweza kupigiwa kura ya turufu na kugeuzwa kuwa sheria ya Uingereza licha ya kupingwa na Baraza la Mabwanyenye kwenye bunge na Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters

Mhariri: Gakuba, Daniel