Waingereza wapiga kura leo | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.05.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waingereza wapiga kura leo

Waingereza wanapiga kura kulichagua bunge jipya. Hata hivyo,mwandishi wetu Christoph Hasselbach anasema uchaguzi huo unahusu siyo tu masuala ya afya,kodi na uhamiaji. Uchaguzi huo ni muhimu kwa mustakabal wa Uingereza.

Ikiwa atashinda katika uchaguzi huo Waziri Mkuu David Cameron ameahidi kuitisha kura ya maoni juu ya Umoja wa Ulaya.

Mwandishi wa DW Christoph Hasselbach

Mwandishi wa DW Christoph Hasselbach

Jee Uingereza iendelee kuwamo katika Umoja huo? Waziri Mkuu Cameron hataweza kurudi nyuma katika hilo,endapo atachaguliwa tena.

Ni kweli kwamba Cameron amesema anataka Uingereza iendelee kuwamo katika Umoja wa Ulaya.

Lakini anataka Umoja wa Ulaya uliofanyiwa mageuzi. Cameron anataka kuona Umoja wa Ulaya usiojiingiza katika masuala ya kitaifa ya wanachama wake, Umoja wa Ulaya usiokuwa na ubadhirifu na ufadhina.

Tabia ya Cameron inakera

Waziri Mkuu Cameron hajatoa mapendekezo yoyote. Bila shaka Cameron atasikia haraka sana kutoka Umoja wa Ulaya kwamba jumuiya hiyo haiwezi kuibadilisha mikataba yake. Pamoja na hayo, viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya wanageukia kwengine inapohusu Waziri Mkuu Cameron. Viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya wanaiona tabia ya Cameron kuwa ya kukera kuhusu masuala ya jumuiya hiyo.

Ni kutokana na tabia yake kwamba Uingereza imepoteza uzito wake wa kisiasa barani Ulaya. Sasa Cameron amenaswa katika mtego. Amewafanya watu wake wawe na matarajio makubwa ya kupatiwa maslahi mazuri kutoka Umoja wa Ulaya.

Ni wazi kwamba hataweza kuyatimiza matarajio hayo. Na inapasa kutilia maanani kwamba chama cha wapinga Umoja wa Ulaya UKIP kimemshupalia.Chama hicho kinaendesha kampeni ya wazi wazi kabisa ya kutaka Uingereza ijitoe kwenye Umoja wa Ulaya.

Sasa Cameron anachochewa na hisia za kuupinga Umoja wa Ulaya,hisia zilizoikumba sehemu kubwa ya jamii ya Uingereza. Ndiyo kusema ,katika muktadha huo, endapo kura ya maoni itafanyika kuamua iwapo Uingereza iendelee kuwamo katika Umoja wa Ulaya ama la, upo uwezekano wa Uingereza kujiondoa kwenye jumuiya hiyo.!

Na jee uamuzi huo utakuwa na athari gani?

Uingereza itaathirika sana kiuchumi lakini ni vigumu kuonyesha hesabu kamili.Na kwa Waziri Mkuu Cameron mwenyewe athari za kisiasa zitakuwa kubwa. Itakumbukwa kwamba mwaka uliopita watu wa Scotland walipiga kura ili kuamua iwapo kuendelea kuwamo katika Umoja wa Uingereza,UK ama la.

Watetezi wa kuwamo katika Umoja walishinda katika kura hiyo ya maoni ,lakini kwa hesabu ndogo. Hata hivyo watu wa Scotland wanaushikilia moyo wa kuipenda Ulaya zaidi kuliko Umoja wa Uingereza.

Ndiyo kusema Scotland inaweza kujitoa kwenye Umoja wa Ufalme wa Uingereza, ikiwa England itajitoa kwenye Umoja wa Ulaya.Lakini Scotland inaweza kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya. Hata hivyo athari za kisiasa na kiuchumi zitakazotokana na Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya hazitaishia ndani ya mipaka ya Uingereza tu.

Wengi katika Umoja wa Ulaya wanasema hawatatoa machozi ikiwa Uingereza itaondoka Umoja wa Ulaya na hakika wanasema mambo yatakuwa mazuri zaidi kwenye Umoja huo bila ya Waingereza kuwamo.Lakini kwa kweli huo ni mtazamao wa hatari!

Ikiwa Uingereza itajiondoa kwenye Umoja wa Ulaya, jumuiya hiyo itapoteza nchi yenye nguvu kubwa za kiuchumi na kifedha na pia itaipoteza nchi ambayo ni mwanachama wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi yenye nguvu za kiatomiki.

Na vyovyote vile matokeo ya uchaguzi yatakavyokuwa nchini Ungereza, wote wale wanaoutetea moyo wa Umoja wa Ulaya nchini Uingereza wanapaswa kusimama pamoja na washirika wao katika Umoja huo ili kuyabainisha mashaka yanayoweza kulikabili bara la Ulaya ikiwa Uingereza itajitoa kwenye Umoja wa Ulaya.

Mwandishi:Hasselbach,Christoph

Mfasiri:Mtullya Abdu.

Mhariri:Gakuba Daniel

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com