Wahanga wa Ebola wanazidi kuongezeka Mashariki mwa DR Kongo | Matukio ya Afrika | DW | 30.08.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Wahanga wa Ebola wanazidi kuongezeka Mashariki mwa DR Kongo

Idadi ya waliokufa kwa Ebola tangu mwaka mmoja uliopita katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imepindukia watu 2,000. Maafisa wa afya wanajitahidi kurejesha imani ya jamii na kukabiliana pia na matatizo ya usalama.

Tume ya serikali inayochunguza jinsi jamii inavyowajibika katika kupambana na maradhi ya Ebola imesema idadi ya kadhia zilizothibitika nayo pia imepanda na kupindukia watu 3000 katika kile kinachoangaliwa kuwa maradhi ya pili hatari yanayoambukiza.

Licha ya kupatikana chanjo na tiba, wauguzi wanapata shida kuyadhibiti maradhi hayo yasienee katika maeneo ya mbali, mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasi ya Congo ambako wakaazi wengi hawaziangalii kwa jicho jema juhudi za kupambana na maradhi hayo.

"Ili dawa iweze kuleta tija, watu wanabidi waikubali na kuwaamini watumishi wa huduma za afya" limesema hayo shirikisho la kimataifa la Msalaba Mwekundu katika taarifa yake.

Mtoto mdogo anachanjwa dhidi ya maradhi ya Ebola katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo

Mtoto mdogo anachanjwa dhidi ya maradhi ya Ebola katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo

Maradhi ya Ebola yanataishia kuenea katika maeneo mengine pia

Hii ni mara ya kumi kwa maradhi ya Ebola kuripuka katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo lakini ni mara ya kwanza kuripuka katika mikoa ya  msongamano wa misitu na milima ya Kivu Kaskazini na Ituri ambako  mapigano ya wanamgambo na mauwaji ya kikabila yamekuwa yakiendelea kwa miongo kadhaa sasa. Hesabu za serikali zinaonyesha idadi ya waliokufa kwa Ebola imefikia watu 2006 na walioambukizwa virusi vya Ebola idadi yao imefikia watu 3004.

Mapema mwezi huu wa Agosti maafisa wa serikali walieneza juhudi zao za kupambana na Ebola katika maeneo mengine na kuzusha hofu huenda maradhji hayo yakatapakaa kwa haraka. Watumishi wa idara za afya wamethibitisha kadhia za mwanzo katika mkoa wa Kivu Kusini Agosti 16 iliyopita. Muda mfupi baadae bibi mmoja akaambukizwa virussi vya Ebola katika eneo la mbali linalodhibitiwa na wanamgambo, Kivu ya kaskazini, umbali wa kilomita mia kadhaa kutoka yale maeneo ambayo yalikuwa tayari yakijulikana kuwa yameambukizwa  na virusi vya Ebola.

"Tunashirikiana na washirika wetu wote ili kuwafikia wananchi, kuwasiliana nao na kuwagundua walioathirika haraka iwezekanavyo" amesema hayo msemaji wa shirika la afya la kimataifa WHO Christian Lindmeier.

Uchunguzi katika maeneo ya mpakani kati ya Congo na Rwanda

Uchunguzi katika maeneo ya mpakani kati ya Congo na Rwanda

Kadhia nyengine ya Ebola yaripotiwa Uganda

 Wakati huo huo wizara ya afya ya Uganda imethibitisha kadhia nyengine ya maradhi ya Ebola imegunduliwa magharibi mwa nchi hiyo na kumuathiri msichana mdogo wa miaka 9 aliyeingia katika eneo hilo akitokea jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/dpa

Mhariri: Grace Patricia Kabogo