1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji 22 wamekufa maji karibu na Pwani ya Ugiriki

28 Machi 2026

Wahamiaji 22 wasio na vibali kutoka Afrika Kaskazini waliokuwa wakijaribu kuelekea Ulaya, wamekufa maji katika eneo lililo nje kidogo mwa Pwani ya taifa la Ugiriki mara baada ya boti yao kuzama.

https://p.dw.com/p/5BJaL
Libya | Wahamiaji wasio na vibali
Boti ya wahamiaji ikifuatiliwa na walinzi wa Pwani ya LibyaPicha: Hazem Turkia/Anadolu/picture alliance

Manusura wa ajali hiyo wamesema boti hiyo dhaifu iliyotengenezwa kwa mpira ilizama siku sita baada ya kuondoka mjini Tobruk nchini Libya.

Walinzi wa Pwani wa Ugiriki wamesema watu 26 akiwemo mwanamke mmoja na mtoto wameokolewa na meli ya shirika linalozisaidia nchi za Ulaya kuilinda mipaka karibu na Kisiwa cha Crete.

Wahamiaji walionusurika ni kutoka Bangladesh na Sudan Kusini

Wamebainisha kuwa walionusurika kufa ni raia 21 wa Bangladesh, wanne wa Sudan Kusini na raia mmoja wa Chad. Boti hiyo iliondoka Libya Machi 21 kuelekea Ugiriki ambako ni kituo kikubwa kwa wahamiaji wasio na vibali wanaotaka kuingia Ulaya.

Mamlaka za Ugiriki zimewakamata wanaume wawili raia wa Sudan Kusini wanaodhaniwa kuwa ni walanguzi wa binadamu na zinawachunguza kwa kuwaingiza wahamiaji nchini humo kinyume cha sheria na kwa kuwasababishia wengine vifo kutokana na uzembe.