WADA: Urusi bado ina kazi ya kufanya | Michezo | DW | 21.11.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

WADA: Urusi bado ina kazi ya kufanya

Maafisa kutoka Shirika la Kimataifa la Kupambana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli – WADA wamesema Urusi haijafanya vya kutosha kurejesha imani ya ulimwengu wa michezo

WADA wamelaani kile wamesema kuwa ni Urusi kushindwa kukiri kuwa iliendesha mpango uliofadhiliwa na serikali wa matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu. Wakizungumza katika mkutano wa Bodi ya WADA mjini Glasgow, walionya kuwa sekta ya michezo nchini Urusi itatatizika kurejesha imani ya ulimwengu wa michezo kama viongozi wake wataendelea kukataa kuyakubali matokeo ya ripoti za uchunguzi uliofichua ufisadi uliokita mizizi. Craig Reedie ni rais wa WADA. "Vipaumbele ni wazi, kama tunaweza kuifanya Urusi kuheshimu na kutekeleza sheria na kanuni, itakuwa habari njema na kama kutakuwa na mchakato ambao kila mmoja anautaka, kile ambacho tumekuwa tukikifanya kwa miaka 17 kikihitaji kutathminiwa basi na tufanye hivyo".

Mkuu wa shirika la kupambana na dawa za kuongeza misuli nguvu la Urusi Vitaly Smirnov aliuambia mkutano huo kuwa serikali ya nchi hiyo haijawahi kujihusisha na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni akisema suala hilo ni tatizo la kimataifa. "Baada ya miaka 10 nilikuwa waziri wa michezo nchini Urusi, na ndani ya Muungano wa Kisovieti. Nilikuwa rais wa Kamati ya Olimpiki ya Urusi kwa miaka 13 hivyo haingewezekana kuchukuliwa aina yoyote ya maamuzi bila ufahamu wangu".

Maafisa wa WADA pia wamelalamikia kile wamesema kuwa ni kuendelea kuzuiwa kufanya vipimo vya matumizi ya dawa hizo na uhalifu wa mtandao dhidi ya shirika hilo.

Hata hivyo Reedie pia alisema kuwa ametiwa moyo kutokana na ukweli kuwa baadhi ya maafisa wakuu wa rusi walikiri kuwa kuna tatizo katika michezo nchini humo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef