1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vurugu zazuka upya Kazakhstan baada ya Urusi kutuma askari

Bruce Amani
6 Januari 2022

Serikali ya Kazakhstan imeweka ukomo kwenye bei ya mafuta kwa muda wa miezi sita. Ni baada ya ongezeko la bei ya mafuta iliyotangazwa mnamo mwaka mpya kusababisha maandamano yaliyokumbwa na vurugu kubwa

https://p.dw.com/p/45DtE
Kasachstan Almaty | Proteste & Ausschreitungen
Picha: Mariya Gordeyeva/REUTERS

Maandamano yameenea katika taifa hilo la Asia ya Kati kutokanana watu kuwa na ghadhabu kuhusu kupanda kwa bei ya petroli wakisema sio haki kutokana na kuwa nchi yao ya Kazakhstan ina hifadhi kubwa ya nishati hiyo.

Soma pia: Urusi yapeleka wanajeshi Kazakhstan kutuliza vurugu

Serikali imesema katika taarifa kuwa imechukua hatua za dharura za kutuliza hali ya kijamii na kiuchumi inayoshuhudiwa nchini humo. Imesema inaweka zuio la siku 180 kwa ongezeko la bei la mafuta katika miji kadhaa na mikoa. Serikali pia imepiga marufuku kwa muda uingizaji wa chakula ikiwemo nyama ya ng'ombe, kondoo, viazi na karoti ili kuweka utulivu wa bei kwa bidhaa za chakula ambazo zina umuhimu mkubwa kwa jamii.

Russland schickt Truppen nach Kasachstan
Urusi imepeleka jeshi la kulinda amani KazakhstanPicha: Russian Defence Ministry/AFP

Vyombo vya habari vinaripoti kutokea kwa milio ya risasi leo jioni katika mji mkubwa wa Almaty wakati vikosi vya usalama vikipambana kutuliza machafuko. Huyu hapa mmoja wa waandamanaji wanaoipinga serikali "Ambieni ulimwengu mzima kitu pekee kinachonawiri nchini Kazakhstan ni rushwa. Kazakhstan imekuwa biashara binafsi ya familia ya raia wa zamani Nazarbayev. Maeneo yote muhimu kimkakati nchini Kazakhstan ni ya familia ya Nazarbayev." Wanajeshi wa Urusi wamewatumwa nchini humo kama sehemu ya jeshi la kulinda amani la Shirika la Mkataba wa Usalama wa Pamoja – CSTO, ambalo ni muungano wa kijeshi unaoongozwa na Urusi wa nchi za zamani za Kisovieti. Kando na Urusi na Kazakhstan, Armenia, Belarus, Kyrgyzstan na Tajikistan pia wanachama wa muungano huo. Mataifa hayo pia yanasemaka kuwa yanawatuma askari wao Kazakhstan, ijapokuwa maelezo ya kiwango cha vikosi hivyo hayajatolewa.

CSTO imesema lengo kuu la ujumbe huo ni kuzilinda taasisi muhimu za serikali na kijeshi. Askari 13 wa Kazakhstan wameuawa mjini Almaty ambapo wawili kati yao walikatwa vichwa. Haijabainika ni raia wangapi waliouawa ijapokuwa vyombo vya habari vinasema madazeni ya washambuliaji waliuawa. Wizara ya afya inasema Zaidi ya watu 1,000 wamejeruhiwa, huku 400 wakilazwa hospitali. Karibu watu 2,000 wamekamatwa mjini Almaty na wengine bado wanaendelea kukamatwa.

Wakati huo huo, wizara ya mambo ya kigeni ya Kazakhstan imekanusha ripoti za vyombo vya habari kuwa raia wa kigeni wamezuiwa kuingia nchini humo. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik. Awali, shirika la habari la RIA liliunukuu ubalozi wa Kazakh nchini Uzbekistan ukisema Kazakhstan hairuhusu kuingia wageni kutokana na maandamano hayo

TUmoja wa Ulaya umetoa wito kwa Urusi kuheshimu uhuru wa Kazakhstan wakati ambapo nchi hiyo imewapeleka askari wake kuzima maandamano makubwa ya kupinga serikali yaliyosababisha ghasia mbaya katika taifa hilo lililokuwa zamani sehemu ya Jamuhuri ya Kisovieti.

Halmashauri Kuu ya Ulaya imesema uko tayari kusimamia mazungumzo ya kuleta amani nchini Kazakhstan.

AFP, DPA