1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wawasili Buenos Aires kwa mkutano wa G20

Daniel Gakuba
30 Novemba 2018

Viongozi wa nchi 20 zilizoendelea zaidi kiuchumi wataanza mkutano wa kilele leo mjini Buenos Aires, Argentina, ambao unatarajiwa kugubikwa na mivutano ya kibiashara, pamoja na mzozo mpya kati ya Urusi na Ukraine.

https://p.dw.com/p/39B8z
Argentinien Buenos Aires G20 Gipfel
Picha: picture-alliance/AP Photo/G. Garello

Rais wa Marekani Donald Trump ni miongoni mwa viongozi ambao tayari wametua mjini Buenos Aires, baada ya kufuta mkutano wake na Rais wa Urusi Vladimir Putin, kutokana mzozo mpya kati ya Urusi na Ukraine katika bahari ya Azov. Kuwepo kwa Trump katika mkutano huo kunapokelewa kwa maoni mchanganyiko, kutokana na sera yake ya Marekani kwanza ambayo imeiweka biashara huria duniani katika hali tete.

Kinachosubiriwa kwa shauku ni mkutano kati ya Trump na rais wa China Xi Jinping, ambao unatazamiwa kutuliza au kuzidisha wasiwasi wa kibiashara. Nchi hizo zinazoogoza kiuchumi duniani zimekuwa na mvutano, na kuwekeana na vikwazo vya kiushuru ambavyo vimeathiri sehemu nyingi za dunia.

Trump asema hataki makubaliano na China

Kabla ya kuanza safari yake, Trump alizungumzia uwezekano wa kupata makubaliano ya China, akisisitiza hata hivyo kwamba hana haraka yoyote, kwa sababu Marekani inanufaika na vikwazo ilivyoiwekea China.

China G20 l US Präsident Donald Trump and Chinesischer Präsident Xi Jinping
Rais wa China, Xi Jinping na Rais wa Marekani, Donald Trump: Mvutano wa kibiashara baina ya nchi zao unagubika mkutano wa G20 mjini Buenos AiresPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Harnik

''Nadhani tunakaribia kupiga hatua na China, lakini sijui kama nataka kufika hapo, kwa sababu sasa hivi Marekani inaingiza mabilioni na mabilioni yatokanayo na ushuru na kodi, kwa hiyo, kusema kweli sijui. Lakini nawaambia, nadhani China wanataka sana kupata makubaliano, na niko wazi kwa makubaliano, lakini kusema kweli napendezwa na hali inavyoendelea.''

Safari ya Trump kutoka Washington hadi Buenos Aires imeandamana na kiwingu cha kisiasa, kufuatia hatua ya aliyekuwa mwanasheria wake binafsi Michael Cohen kukiri mahakamani, kwamba alilidanganya bunge kuhusu mipango ya kibiashara ya kampuni ya Trump nchini Urusi.

Suali linaloulizwa na wengi ni ikiwa Trump atakutana na Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman, anayeshukiwa kuhusika katika mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi.

Ndege ya Merkel yapata hitilafu

Deutschland Flughafen Köln/Bonn - Kanzlerin Merkel muss Flug zu G20 unterbrechen
Ndege ya Kansela Merkel ililazimika kukatiza safari baada ya mawasiliano yake kukatika ghafla.Picha: Reuters/A. Rinke

Wakati viongozi wengine wangi wakiwa tayari wamewasili nchini Argentina, wakiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza na Rais wa Ufaransa, Kansela wan Ujerumani Angela Merkel yumkini atakosa sherehe za ufunguzi wa mkutano huo muhimu, kwa sababu ndege yake, Airbus ''Konrad Adenauer'' ililazimika kukatisha safari hapo jana ikiwa juu ya anga ya Uholanzi na kutua kwenye uwanja wa Cologne na Bonn, baada ya marubani wa ndege hiyo kubaini hitilafu katika mfumo wa mawasiliano.

Hata hivyo, gazeti la Bild la hapa Ujerumani limewanukuu marubani wa ndege hiyo, wakisema haikuwa katika kitisho chochote cha usalama. Lakini, gazeti jingine la Rheinische Post limeripoti kuwa wachunguzi wataangalia pia uwezekano wa sababu za kihalifu katika masaibu yaliyoikumba ndege hiyo.

 

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, rtre, ape

Mhariri: Grace Patricia Kabogo