1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya maisha ya kawaida yabadilika Ulaya kufuatia Corona

Saumu Mwasimba
16 Machi 2020

Masuala muhimu kwenye kwenye meza ni jinsi ya kuzuia maambukizi zaidi,kusambaza vifaa tiba na kuimarisha utafiti

https://p.dw.com/p/3ZWmS
Coronavirus - Sitzung des EU-Parlaments in Brüssel
Picha: AFP/K. Tribouillard

Halmashauri kuu  ya Umoja wa Ulaya imesema hatua ya kufunga mipaka sio njia bora ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona katika umoja huo. Kauli hiyo imetolewa leo wakati nchi mbali mbali za bara hilo ikiwemo Ujerumani zikichukua hatua hiyo miongoni mwa nyingine. 

Tukianzia hapa barani Ulaya viongozi wanajiandaa kufanya mkutano wa kilele wa dharura kesho Jumanne kwa njia ya vidio  kuhusiana na hali ilivyo mpaka kufikia sasa kuhusu ugonjwa huo wa virusi vya Corona.

Rais wa baraza la Ulaya Charles Michel akitoa taarifa amesema suala muhimu linaloangaziwa na umoja huu kwa sasa ni jinsi ya kuzuia kuenea kwa maambukizi, kusambaza vifaa tiba zaidi pamoja na kuimarisha utafiti na kuzuia athari za kiuchumi zinazoweza kusababishwa na ugonjwa huo.

Schweiz | Fiona Furrer vom Medizinischen Fachpersonal: COVID-19-Abstrich in häuslicher Umgebung
Picha: picture-alliance/KEYSTONE/E. Leanza

Viongozi hao wa Ulaya wanakutana wakati kila nchi ikiwa imezidi kuchukua hatua ya kujaribu kukabiliana na kusambaa kwa ugonjwa huo ikiwemo kufunga mipaka, shule, mikahawa na kuweka sheria kali katika masuala mengine ya shughuli za kijamii. Ugiriki mojawapo ya nchi zilizoko ndani ya Umoja wa Ulaya imethibitisha visa 331 vya watu walioambukizwa virusi vya Corona na watu wanne wameshakufa kutokana na virusi hivyo.

Nchi hiyo imefikia uamuzi wa kufunga maduka yote ya reja reja kuanzia siku ya Jumatano. Lakini pia mji mkuu Athens umepiga marufuku meli zote za usafiri wa abiria kutoka Italia kutia nanga kwenye bandari zake.

Nchini Uswizi nako hatua mbali mbali zimechukuliwa ikiwemo kufutiliwa mbali kwa vikao vya bunge la taifa. Nchi hiyo imeripoti visa  vipya jumla ya 840 kufikia jana Jumapili na kuifanya idadi hiyo ya wenye virusi vya Corona nchini humo kufikia watu 2,200 sawa na idadi iliyorekodiwa katika nchi jirani yake ya Liechtenstein.

Russland Moskau | Coronavirus | Desinfektion Öffentliche Verkehrsmittel
Picha: Reuters/T. Makeyeva

Idadi hiyo imetajwa kuwa ni zaidi ya asilimia 50 kwa siku moja hali ambayo inaonesha kwamba maambukizi ya ugonjwa huo yanaongezeka kwa kasi kubwa. Kadhalika barani Ulaya mashirika mengi makubwa ya ndege yametangaza leo Jumatatu yatapunguza safari zao kwa hadi asilimia 90 kufuatia kushuka kwa idadi ya wateja.

Mashirika ya Air France na KLM yamesema yamechukua hatua hiyo kutokana na sheria za kuzuiwa wasafiri wengi kutoka Ufaransa, Uholanzi  na nchi nyingine nyingi za Ulaya. Katika eneo la Mashariki ya Kati Iran imesema virusi vya Corona vimeuwa watu wengine 129 na kuifanya idadi ya waliokufa kwa ugonjwa huo nchini humo kufikia 853 huku waliothibitika kuambukizwa wakifikia 14,991. Iran inapambana kujaribu kuzuia kusambaa kwa mripuko huo ingawa idadi hiyo ya waliokufa leo ndio idadi kubwa zaidi tangu lilipozuka janga hilo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo