1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu waomboleza kifo cha kiongozi wa upinzani Navalny

Sylvia Mwehozi
17 Februari 2024

Viongozi wa Ulimwengu na wanaharakati wa upinzani wa Urusi, wameendelea kumlaumu rais Vladimir Putin na serikali yake kwa kifo cha kiongozi wa upinzani Alexei Navalny aliyefia gerezani.

https://p.dw.com/p/4cVk8
Russland Navalny Demo Portrait
Picha: Sefe Karacan/AA/picture alliance

Viongozi wa Ulimwengu na wanaharakati wa upinzani wa Urusi, wamemlaumu rais Vladimir Putin na serikali yake kwa kifo cha kiongozi wa upinzani Alexei Navalny aliyefia gerezani.

Rais wa Marekani Joe Biden amesema Washington haijui ni nini hasa kimetokea, lakini hakuna shaka kwamba kifo cha Navalny ni matokeo ya njama za Putin na genge lake.

Biden ameongeza kwamba Navalny "angeweza kuishi salama uhamishoni," lakini badala yake akarejea

Urusi "kuendeleza kazi yake," licha ya kujua kwamba anaweza kufungwa au kuuawa "kwa sababu anaamini sana katika nchi yake, nchini Urusi."

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, ambaye nchi yake ilimpokea kwa muda Navalny mnamo 2020 baada ya kuwekewa sumu, alisifu ushujaa wa mkosoaji huyo wa Kremlin na kusema kifo chake kinaonyesha wazi "ni aina gani ya utawala huo."

Naye Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ambaye yuko Ujerumani kuhudhuria mkutano wa usalama wa Munich, amesema ni wazi kwamba mwanasiasa huyo ameuawa na Putin. "Putin hajali nani anakufa, mradi tu yeye ashikile nafasi yake".

Soma: Mpinzani wa Putin Navalny ahamishiwa gereza Aktiki

Serikali ya Uingereza ilisema Ijumaa jioni kwamba imewaita wanadiplomasia kutoka ubalozi wa Urusi "kuweka wazi kwamba inaziwajibisha mamlaka za Urusi kikamilifu" kwa kifo cha mkosoaji wa Kremlin Alexei Navalny.

Wafuasi wa Navalny wamejitokeza katika miji ya barani Ulaya siku ya Ijumaa ili kumuenzi mwanasiasa huyo anayetambulika kama kiongozi mkuu wa upinzani nchini Urusi, hata alipokuwa gerezani.

Kifo chake kilitangazwa mapema jana na maafisa wa gereza la Arctic la Urusi ambako alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 19 jela.