1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Israel,Misri na UAE wakutana kwa mara ya kwanza

Saumu Mwasimba
22 Machi 2022

Mazungumzo yao yakilenga zaidi kuhusu utulivu wa soko la nishati  pamoja na usalama wa chakula miongoni mwa mengine

https://p.dw.com/p/48sx4
Ägypten Griechenland G20 Gipfel
Picha: John Macdougall/AP Photo/picture alliance

Rais wa Misri AbdelFatah al Sissi, waziri mkuu wa Israel Naftali Bennett pamoja na mrithi wa Ufalme wa Umoja wa Falme za Kiarabu Mohammed bin Zayed wamekutana katika eneo la kitalii la Sharm el Sheikh nchini Misri na kujadiliana kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa.

Mazungumzo yao yakilenga zaidi kuhusu utulivu wa soko la nishati  pamoja na usalama wa chakula. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais wa Misri leo Jumanne.

Mtawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu Mohammed bin Zayed  aliwasili Misri akiongoza ujumbe wake wa kiserikali mnamo Jumatatu na kukutana na rais Al Sisi wa Misri ambapo majadiliano yao yalituwama kwenye suala la ushirikiano baina ya nchi zao.

Vereinigte Arabische Emirate | Besuch Premierminister Boris Johnson
Picha: Stefan Rousseau/AP/picture alliance

UAE pamoja na Saudi Arabia zimekataa  kuongeza uzalishaji mafuta licha ya kutakiwa kufanya hivyo na nchi za Magharibi kufuatia kukupanda kwa bei katika soko la   nishati ya mafuta ghafi hali iliyochochewa na hatua ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Waziri mkuu wa Israel Bennett nae aliwasili Misri Jumatatu kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na ofisi yake hii ikiwa ni ziara yake ya pili nchini Misri . Aliwahi kukutana na rais Al Sissi mnamo mwezi Septemba katika eneo hilo la Sharm el Sheikh.

Lakini huu ni mkutano wa kwanza wa pamoja wa viongozi hao watatu tangu Umoja wa Falme za kiarabu uliposaini makubaliano yaliyosimamiwa na Marekani ya kuanzisha ushirikiano rasmi na  Israel mnamo mwaka 2020.

Vereinigte Arabische Emirate Dubai | Baschar al-Assad trifft Kronprinz Mansour bin Zayed Al Nahyan
Picha: Syrian Presidency Facebook page/AP/picture alliance

Mkutano huo wa Jumanne huko Misri umekuja siku chache baada ya rais wa Syria Bashar al Assad kukutana na mtawala wa UAE katika ziara yake ya kushtukiza nchini Emarati. Misri ilikuwa nchi ya kwanza ya kiarabu kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel mnamo mwaka 1979.