1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yajaribu kupambana na mgogoro wa kiuchumi

Amina Mjahid
13 Agosti 2018

Benki kuu ya Uturuki imejaribu kurejesha utulivu katika masoko ya hisa yalioshuhudia kuporomoka kwa thamani ya sarafu ya Uturuki ya Lira huku rais Tayyip Erdogan akiikaripia Marekani kuiendea kinyume nchi yake.

https://p.dw.com/p/33633
Türkei 1. Jahrestag nach Putschversuch Präsident Erdogan
Picha: Reuters/U. Bektas

Mgogoro kati ya washirika wa Jumuiya ya kujihami ya  NATO, Uturuki na Marekani, uliofikia kiwango kipya baada ya kukamatwa mchungaji wa Kimarekani  Andrew Brunson, umesababisha kuporomoka kwa thamani ya sarafu ya Uturuki na kuzua masuali mengi ya kuuliza juu ya mahusiano ya baadae ya nchi hizo hasimu. Wakati matukio ya hivi karibuni yakisababisha thamani ya sarafu hiyo kushuka waekezaji wana wasiwasi juu ya uchumi wa Uturuki na hasa katika benki ya Ulaya.

Türkei, Symbolfoto: Währung Türkische Lira
Pesa za Uturuki-Lira Picha: picture-alliance/dpa/C. Merey

Sarafu ya Lira ambayo imeshaporomoka ilizidi kushuka kwa asilimia 16 dhidi ya dola ya kimarekani siku ya Ijumaa wakati rais Donald Trump alipotangaza kuongeza mara mbili ushuru katika bidhaa za chuma na bati kutoka Uturuki. "Tuko pamoja katika Jumuiya ya kujihami ya NATO kisha unatafuta njia za kumsaliti au kumuendea kinyume mshirika mwenzako, kitu kama hiki kinaweza kukubalika kweli?" Alisema rais Tayyip Erdogan wakati alipokutana na mabalozi wa Uturuki mjini Ankara hii leo.

Rais huyo wa Uturuki amesema anaamini thamani ya Lira itarejea kuwa imara zaidi hivi karibuni.

Awali benki kuu ya Uturuki ilisema iko tayari kuchukua hatua zozote zinazohitajika ili kuhakikisha kunakuwepo na unafuu wa kiuchumi huku ikiahidi kutoa ukwasi kwa mabenki nchini humo kupambana na mgogoro wa kiuchumi uliopo. Lakini taarifa hiyo haikuelezea chochote juu ya kupandishwa viwango vya riba vinavyohitajika kuimarisha thamani ya lira.

NATO yasema haitoingilia mgogoro wa kidiplomasia wa wanachama wake

Huku hayo yakiarifiwa Waziri wa fedha wa Uturuki Berat Albayrak amemsifu waziri mwenzake wa Ujerumani hii leo Jumatatu aliekosoa ushuru mkubwa Marekani ulioweka kwa bidhaa za chuma na bati kutoka Uturuki. Waziri Albayrak amesema kutetea diplomasia kutaimarisha mahusiano mazuri kati ya nchi yake na Ujerumani pamoja na Umoja wa Ulaya. 

USA Donald Trump zum Atomdeal mit Iran
Rais wa Marekani Donald Trump Picha: Reuters/J. Ernst

Waziri huyo wa fedha wa Uturuki aliyasema hayo kupitia matamshi yake alioyaweka katika mtandao wake wa kijamii wa twitter baada ya waziri wa Uchumi wa Ujerumani Peter Altmaier  aliesema ongezeko la ushuru kutoka serikali ya rais Trump na sera za vikwazo zinaharibu ajira pamoja na maendeleo. Ameongeza kuwa Ulaya haitokubali shinikizo la Marekani juu ya Iran.

Shirika la kujihami NATO limesema halina nia ya kuingilia vita au mgogoro wa kidiplomasia uliopo hivi sasa kati ya Marekani na Uturuki ambao wote ni wanachama wake.  Afisa mmoja wa NATO amesema kile kinachoendelea kwa sasa ni msuala ya mahusiano na haihusiki hata kidogo.

Afisa huyo amedai kuwa mara kwa mara wanachama wa NATO hutofautiana lakini licha ya hayo washirika wameweza kukubaliana kusimama pamoja na kulindana.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman