Usalama waimarishwa Uganda Bobi Wine akisubiriwa kurudi | Matukio ya Afrika | DW | 20.09.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Usalama waimarishwa Uganda Bobi Wine akisubiriwa kurudi

Robert Kyagulanyi, maarufu kwa jina la Bobi Wine, anatarajiwa kurudi nyumbani leo kutoka Marekani ambako alikwenda kwa matibabu. Polisi wameanza kuwakamata watu kabla ya mbunge huyo, mkosoaji wa rais Museveni kurejea.

Polisi nchini Uganda wameanza kuwakamata watu hovyo kabla ya kurejea nyumbani kwa msanii na mbunge mashuhuri wa upinzani, Robert Kyagulanyi, nchini humo hivi leo.

Kyagulanyi, maarufu kwa jina la Bobi Wine, anatarajiwa kurudi nyumbani leo  kutoka Marekani ambako alikwenda kwa matibabu, kutokana na kile alichodai ni kuteswa na maafisa wa usalama alipokuwa rumande.

Polisi wamemkamata ndugu wa mwimbaji huyo na watu wengine wawili wakati wakisafiri kwa gari kuelekea uwanja wa ndege. Wakili Asuman Basalirwa  amesema polisi hawakutoa sababu ya kukamatwa kwao.

Mbunge mwengine wa upinzani Medard Sseggona amesema aliwakimbia polisi waliofika nyumbani kwake  kwa lengo la kumtia nguvuni. Polisi pia waliizingira nyumba ya Meya wa Kampala, Erias Likwago.

Kyagulanyi, mpinzani mkubwa wa Rais Yoweri Museveni, anatarajiwa kuwasili Uganda mchana huu. Polisi wamepiga marufuku mikusanyiko yote ya hadhara.