1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yakataa uchunguzi wa kimataifa kuhusu kifo cha Navalny

Tatu Karema
20 Februari 2024

Ikulu ya Kremlin imepinga ombi la Umoja wa Ulaya la uchunguzi wa kimataifa kuhusu kifo cha kiongozi wa upinzani Alexei Navalny

https://p.dw.com/p/4ccY3
Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov akizungumza wakati wa hafla ya tuzo ya Urusi kwa uaminifu kwa sayansi mjini Moscow mnamo Oktoba 26, 2023
Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry PeskovPicha: Mikhail Tereshchenko/TASS/dpa/picture alliance

Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema kwamba Urusi haiwezi kutimiza ombi hilo la Umoja wa Ulaya na kwamba inachukulia hatua hiyo kama muingilio wa masuala ya ndani ya nchi hiyo. Haya ni kulingana na vyombo vya habari vya Urusi.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alikuwa ametoa wito wa uchunguzi huo wa kimataifa lakini msemaji wa Navalny amesema kuna matumaini madogo ya Urusikuachilia mwili wa kiongozi huyo wa upinzani kwa mkewe ama mamake katika siku za hivi karibuni.

Peskov asema madai kwamba Putin amemuua Navalny hayana msingi

Kuhusiana na madai ya Navalnaya kwamba Putin amemuua mumewe, Peskov amesema kwamba  madai hayo hayana msingi kabisa na ni mashtaka makali dhidi ya mkuu wa serikali ya Urusi, lakini akaongeza kwamba kwa kuzingatia Yulia Navalnaya amekuwa mjane siku chache zilizopita, hatozungumzia suala hilo.

Soma pia:Mjane wa Navalny aahidi kuendeleza kazi yake

Katika ujumbe aliyotuma kwa njia ya video siku ya Jumatatu, Navalnaya alimlaumu Putin kwa kifo cha Navalny katika gereza moja ya kikoloni nchini humo na kutangaza kwamba ataendelezea vita vya mumewe dhidi ya mfumo wa urais wa Urusi.

Kiongozi wa upinzani wa Urusi Alexei Navalny akiwa mahakamani mjini Moscow mnamo Agosti 27, 2018
Kiongozi wa upinzani wa Urusi Alexei Navalny Picha: Pavel Golovkin/AP Photo/picture alliance

Peskov amesema kwamba yeye na Rais Putin hawajatazama video hiyo.

Navalnaya autaka Umoja wa Ulaya kutotambua matokeo ya uchaguzi wa Urusi

Katika hatua nyingine, Navalnaya, ameutaka Umoja wa Ulaya kutotambua matokeo ya urais ya uchaguzi wa Machi nchini Urusi.

Kulingana na nakala ya hotuba yake iliyotolewa na msemaji wake mmoja, Navalnaya ameliomba baraza la mambo ya nje la Umoja wa Ulaya kutotambuwa uchaguzi huo.

Hotuba hiyo imeendelea kusema kwamba Rais aliyemuuwa mpinzani wake mkuu hawezi kutambulika kuwa halali.

Putin ameonya kwamba kutakuwa na majibu makali ikiwa mataifa ya kigeni yatajaribu kuingilia uchaguzi wa Urusi.

Ufaransa na Ujerumani zawaita mabalozi wa Urusi kuhusiana na kifo cha Navalny

Ufaransa inatarajia kumuita balozi wa Urusi mjini Paris leo jioni kufuatia mauaji ya Navalny. Haya yameripotiwa na gazeti la Le Monde lililonukuu matamshi ya waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Stephane Sejourne aliyekuwa ziarani nchini Argentina.

Hapo jana Jumatatu, Ujerumani pia ilimuita balozi wa Urusi mjini Berlin kuhusiana na kifo hicho cha Navalny.

Ukraine yataka vikwazo zaidi dhidi ya Urusi

Waziri mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal, ameuhimiza Umoja wa Ulaya na Japan kuweka vikwazo vipya vya kiuchumi dhidi ya Urusi baada ya kifo cha Navalny.

Matamshi hayo yanakuja baada ya mataifa ya Umoja huo kama vile Ujerumani, Lithuania na Sweden kutafuta adhabu mpya maalum kufuatia kifo hicho cha Navalny.